………………..
Na Happy Lazaro, Arusha
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,amefunga rasmi mkutano wa Nne wa Kamisheni ya Kudumu ya Ushirikiano baina Tanzania na Zambia kuhusu masuala ya Ulinzi na Usalama (Joint Permanent Commission on Defence and Security -JPCDS) uliofanyika  kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 23 hadi 27 Februari, 2026 katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha.
Tanzania na Zambia zimesaini makubaliano ya kuendelea kuimarisha ulinzi,kubadilishana taarifa za kiintelijensia pamoja na uhusiano wa kiuchumi kwa wananchi wake kufanya biashara salama bila vikwazo vyovyote.
Akizungumza jijini Arusha wakati wa mkutano wa nne  wa kudumu baina ya Tanzania na Zambia Waziri wa Ulinzi, na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Rhimo Nyansaho amesema lengo ni kubadilishana uzoefu katika masuala ya ulinzi,intelijensia,kudhibiti wahamiaji haramu pamoja na uhalifu
Kaimu Waziri wa Ulinzi ambaye pia ni Waziri wa Ndani Zambia , JACOB MWIIMBU,amesema Tanzania ni nchi salama na ndiyo maana uhusiano umedumu kwa miaka mingi hasa kiuchumi kwa kupitia reli ya Tazara na kuwaonganisha wafanyabiashara.
Nchi hizo mbili za Tanzania na Zambia hukutana kila mwezi Febuari kwa lengo la kujadili mafanikio na changamoto zilizopo na kuzipatia majibu.
Mkutano huo ulianza na ngazi ya wataalamu ambapo uliendeshwa kwa muda wa siku tano, wakiongozwa na Makatibu Wakuu wa Sekta ya Ulinzi kutoka Serikali zote mbili, ambapo waliweza kufanya mapitio ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa tatu uliopita ambao uliofanyika Livingstone, Zambia Mwaka 2025, pamoja na kuweka maazimio mapya kabla ya kufikishwa ngazi ya mawaziri kwa hatua ya mapitio zaidi.
Aidha Mkutano huo pia uliwashirikisha Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutoka Nchi zote mbili, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zambia ambapo mkutano huo pia, ulipokea na kujadili ripoti kutoka Kamati zote tatu ikiwemo ya Ulinzi, Usalama wa ndani pamoja na ile ya Usalama wa Taifa na kuweka msisitizo kuhusu kuwepo haja ya kuhakikisha kuwa maazimio yote yaliyotakiwa yanatekelezwa.