Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma 

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kuwa wizara haitavumilia viongozi na watendaji wasiofanya kazi huku wananchi wakikosa huduma ya maji safi na salama, akisisitiza kuwa isiyotekeleza wajibu wake itawajibishwa kulingana na taratibu husika.

Aweso ameyasema hayo Februari 27, 2026 , jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa RUWASA na Vyombo vya Utoaji Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs).

Amesema kuwa msingi wa utoaji huduma ukiwa imara, wizara itaweza kusimamia sera na kutekeleza miradi ya kimkakati badala ya kushughulikia malalamiko ya mara kwa mara kutoka ngazi ya chini. 

Aidha amebainisha kuwa wizara imeanza tathmini kuanzia ngazi ya chini kabisa na itachukua hatua kali kwa watakaobainika kushindwa kusimamia rasilimali za miradi ya maji, Ameongeza kuwa hawatakubali kuona viongozi hawajui mapato, matumizi na salio la fedha huku wananchi wakihangaika kupata maji, akisisitiza kuwa ukusanyaji na matumizi ya fedha lazima yawe wazi na yenye tija kwa jamii.

Kuhusu uendeshaji wa miradi, amesema kuwa haiwezekani wananchi wakose maji kwa sababu ya kuishiwa LUKU wakati wahusika walijua mapema mahitaji ya umeme. Aidha amebainisha kuwa wataalamu wakiwemo wahasibu na mafundi wanapaswa kuzingatia utaalamu wao na kutoa taarifa mapema ili kuhakikisha huduma haikwami.

Aweso amesema kuwa wizara inahitaji watendaji wanaosema “inawezekana” na wanaotekeleza majukumu kwa matokeo yanayopimika, akionya kuwa maneno matupu hayataleta maendeleo katika sekta ya maji.‎Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri, amewataka watumishi kila mmoja kuzingatia utaalamu wake katika utekelezaji wa kazi. Aidha amebainisha kuwa watendaji hawapaswi kufanya kazi kwa mazoea bali kwa kuangalia muktadha mzima wa uendeshaji wa utoaji huduma ili kuhakikisha huduma inakuwa yenye ufanisi na tija kwa wananchiKwa upande wake, Mwenyekiti wa CBWSOs, Bw. Nicolaus Kombe, amesema kuwa vyombo hivyo vinaendelea kutoa huduma kwa kufuata miongozo ya wizara na RUWASA. Aidha ameongeza kuwa gharama za uendeshaji na vipuri zimepanda huku tozo zikibaki palepale, hivyo ameomba wizara ya kutekeleza mpango wa biashara ulioandaliwa miaka mitatu iliyopita ili kuboresha utoaji wa huduma.

Amebainisha kuwa watumishi wa vyombo hivyo hawana mfumo rasmi wa ajira na maslahi yao si mazuri, akiomba wizara kuharakisha utaratibu wa kuwawezesha kupata mfumo utakaowalinda hadi wanapostaafu, huku akiahidi kuendelea kutekeleza maelekezo yote yanayotolewa ili wananchi waendelee kupata maji safi na salama.