NA EMMANUEL MBATILO
Mpaka sasa Tanzania Red Cross Society (TRCS) imeweza kushiriki kukabiliana na maafa mbalimbali hususani mafuriko sehemu mbalimbali hapa nchini, ambapo imeweza kuwahudumia familia zisizopungua 2,895 kwa kuwapatia vifaa vya kujikimu na familia 454 kusaidiwa fedha.
Ameyasema hayo leo Rais wa Tanzania Red Cross, Bw.David Kihenzile baada ya kukaa kikao na baadhi ya wadau mbalimbali wa Makao mkuu ya shirika hilo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katka kikao hicho Bw.Kihenzile amesema wamekuwa na utayari wa kukabiliana na maafa kwa kuwaanda Voluntia ama vikosi kazi kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali na kuandaa vifaa.
“Mpaka sasa tumejenga ghala Jijini Dodoma lakuhifadhia vifaa lenye ukubwa wa mita za mraba 600, ambapo sasa ni rahisi kutoka Dodoma kwenda Mkoa wowote wenye uhitaji vifaa”. Amesema Bw.Kihenzile.
Aidha amesema wamekuwa wakitoa huduma kwa jamii hasa maji, usafi wa mwili na mazingira katika wilaya za Buhigwe Mkoani Kigoma na Simanjiro Mkoani Manyara,
Pamoja na hayo Bw.Kihenzile amesema kuwa wamekuwa wakishiriki kampeni mbalimbali hapa nchini ikiwemo Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Luberea mwaka 2019 na kutoa elimu ya afya kwa jamii kwenye kampeni hiyo.
Hata hivyo amesema wameweza kusaidia kuboresha maisha ya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu mkoani Shinyanga ambapo zaidi ya Walezi 55,000 wananufaika na mradi ambapo watoto hao (OVC) wanapelekwa kwenye mafunzo VETA na kusaidia uniform na vifaa vya shule.
Mwisho ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za shirika hilo ili liendelee kutimiza majukumu ya huduma ambazo zinatolewa na shirika hilo.