Na John Bukuku, Fullshangwe Media
Februari, 2026
Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ilala amesema ofisi hiyo imefanikiwa kudhibiti zaidi ya Shilingi bilioni 1.5 katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2025, kufuatia uchambuzi wa mifumo ya uwasilishaji wa michango ya hifadhi ya jamii kwa waajiri wa sekta binafsi.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, amesema jumla ya Shilingi 1,533,241,211.36 zimedhibitiwa baada ya kufanyika kwa uchambuzi wa mfumo wa uwasilishaji wa michango ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa waajiri 71 wa sekta binafsi.
Alisema katika uchambuzi huo ilibainika kuwa idadi kubwa ya waajiri hawakuwa wanawasilisha michango ya wafanyakazi kwa mujibu wa sheria, hali iliyokuwa ikiathiri haki za wafanyakazi. Hata hivyo, baada ya TAKUKURU kuingilia kati, fedha hizo tayari zimewasilishwa katika mfuko wa NSSF kwa manufaa ya wafanyakazi husika.
Amesema uchambuzi wa mifumo ya utendaji kazi na utoaji huduma hufanyika kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa na baadaye kushauri namna bora ya kuiziba ili kuondoa vitendo vya rushwa na kuongeza ufanisi, huku akibainisha kuwa ufuatiliaji huo ni endelevu na waajiri wanapaswa kuzingatia sheria kwa kuwasilisha michango kwa wakati.
Aidha, ameeleza kuwa katika mashauri yanayohusiana na ubadhirifu, baadhi ya watuhumiwa walirejesha Shilingi 64,750,000, huku mashauri mengine tisa yakiendelea katika mahakama mbalimbali.
Kwa upande wa mikakati ya Januari hadi Machi, 2026, amesema TAKUKURU (M) Ilala itaweka mkazo katika kufuatilia matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ili kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinatumika ipasavyo na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Pia amesema ofisi hiyo itaendelea kutoa elimu kwa jamii na makundi mbalimbali, hususan wanafunzi, kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili, uadilifu na uzalendo kwa Taifa.
Akimarizia, Naibu Mkuu huyo wa TAKUKURU (M) Ilala amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji ushirikiano wa wananchi wote, akieleza kuwa kuzuia rushwa ni jukumu la kila mmoja na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo ili kuwezesha ustawi wa kijamii kupitia miradi bora ya maendeleo na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
