Rachel Kaduma Kaimu Mkurugenzi idara ya uendelezaji miji na vijiji- TAMISEMI  amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa Green and Smart Cities unaendelea katika hatua mbalimbali kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi, kuongeza fursa za ajira kwa vijana pamoja na kuimarisha huduma za kijamii katika maeneo ya mijini.

Akizungumza katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi huo, mkurugenzi huyo alisema mradi unahusisha ukarabati na uboreshaji wa maeneo ya uvuvi, pamoja na kuwajengea uwezo vijana kupitia mafunzo ya ufundi katika vyuo vya VETA. Mafunzo hayo yanawasaidia vijana kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kupata ajira katika sekta mbalimbali za kiuchumi.

Alieleza kuwa lengo jingine la mradi huo ni kuhakikisha miji inakuwa safi na yenye mazingira rafiki kwa wananchi, ambapo huduma muhimu zinaboreshwa ili wananchi waweze kupata huduma bora na kwa urahisi.

Pia alisema kikao hicho kimeandaliwa ili kujadili changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi na kutoa mapendekezo yatakayowasilishwa kwa viongozi wa juu kwa ajili ya kufanya maamuzi.

“Tunapitia changamoto mbalimbali lakini pia tunapata fursa ya kubadilishana uzoefu kati ya wadau. Wale ambao wamefanikiwa katika maeneo yao wanashirikisha wenzao mbinu walizotumia ili kuboresha utekelezaji wa mradi,” alisema.

Kwa upande wa wanufaika wa mradi huo, Mratibu wa Programu ya Green and Smart Cities katika Manispaa ya Ilemela, Ahmed Sakif, alisema programu hiyo inafadhiliwa na European Union kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

Alieleza kuwa mradi huo ulianza mwaka wa fedha 2022/2023 na unatekelezwa katika halmashauri mbalimbali zikiwemo Mwanza na Tanga.

Sakif alisema mradi huo una maeneo makuu matatu ya utekelezaji ambayo ni msaada wa kibajeti kwa halmashauri, uboreshaji wa miundombinu kama masoko na mialo ya samaki, pamoja na uhifadhi wa mazingira na rasilimali maji.

Aliongeza kuwa kupitia mradi huo vijana zaidi ya 600 wamepata mafunzo ya ufundi katika vyuo mbalimbali na wanatarajiwa kuunganishwa na fursa za mitaji ili kuanzisha shughuli za kujiajiri.

Kwa ujumla, wadau wa mradi huo wamesema kuwa hatua zilizofikiwa hadi sasa zinaonesha mafanikio makubwa, huku wakisisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali, mashirika ya maendeleo na wananchi ni muhimu ili kuhakikisha mradi unaleta matokeo chanya kwa jamii.

Mwakilishi kutoka Umoja wa Ulaya, Jorginsen, amesema kuwa ujumbe wa EU nchini Tanzania unatekeleza programu ya Green and Smart Cities SASA kwa kushirikiana na serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu.

Alieleza kuwa programu hiyo inalenga kusaidia maendeleo endelevu katika miji ya Tanzania, hususan katika miji ya sekondari, kwa kuboresha huduma muhimu kama maji safi na usafi wa mazingira. Kazi kubwa imefanyika katika maeneo ya Unguja na Pemba kwa kushirikiana na watumishi wa serikali za mitaa pamoja na taasisi za maji.

Katika utekelezaji wake, programu hiyo imefanikiwa kusaidia upanuzi wa miundombinu ya maji na usafi wa mazingira, ikiwemo kuboresha huduma katika Jiji la Manta, na sasa wanaendelea na awamu ya pili na ya tatu ya mradi huo. Pia kuna mipango ya kuanzisha miradi kama hiyo katika mji wa Tanga ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zaidi za msingi. Lengo kuu ni kuongeza upatikanaji wa huduma bora huku miji ikiendelea kukua kwa njia endelevu.

“Mbali na sekta ya maji, programu hiyo pia inashughulikia maendeleo ya masoko na biashara ndogo ndogo kupitia mpango wa Inclusivity,” amesema.

Amesema kupitia mpango huo, vijana na wanawake wanapewa fursa ya kuimarisha biashara zao ndogo na kuongeza kipato. Programu hiyo pia inaunganisha wajasiriamali hao na masoko ndani ya miji ili kusaidia kukuza uchumi wa ndani na kuongeza ajira.

Aidha, ushirikiano umefanywa na taasisi mbalimbali kama vile zile zinazohusika na fedha, mafunzo ya ufundi stadi na ujenzi wa uwezo kwa watumishi wa serikali za mitaa.

Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa taasisi za ndani zinaimarishwa ili ziweze kuendelea kusimamia miradi hiyo hata baada ya programu kukamilika.

Jorginsen alisisitiza kuwa kujenga uwezo wa taasisi ni sehemu muhimu ya kuhakikisha miradi hiyo inadumu kwa muda mrefu.