Mwandishi wa vitabu vitano vya anatomia vinavyoendana na mtaala wa sasa ya Udaktari Profesa wa Anatomia wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) David Ngassapa akishika Kitabu cha Histology kinachomsaidia mwanafunzi wa udaktari kujifunza namna ya kuchunguza mwili wa binadamu kwa kutumia darubini na kutambua muonekano wa sehemu mbalimbali za mwili, ikiwemo ngozi na mifupa wakati akizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 25, 2026, jijini Dar es Salaam (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Mwandishi wa vitabu vitano vya anatomia vinavyoendana na mtaala wa sasa ya Udaktari Profesa wa Anatomia wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) David Ngassapa, akizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 25, 2026, jijini Dar es Salaam kuhusu umuhimu wa vitabu hivyo katika kuwafundisha wanafunzi wa fani ya udaktari.
Kaimu Rasi wa Ndaki ya Tiba wa MUHAS, Profesa Agricola Joachim a kizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 25, 2026, jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa baadhi ya vitabu vya anatomia vinavyotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
…………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kinatarajia kuzindua vitabu vitano vya anatomia vinavyoendana na mtaala wa sasa, vinavyolenga kuongeza uelewa kwa wanafunzi wa fani ya udaktari. Hatua hiyo itasaidia kukabiliana na changamoto ya uhaba wa vitabu vya kujifunzia pamoja na kuongeza ufanisi katika kuzalisha wahitimu wenye umahiri.
Vitabu hivyo ni pamoja na Human Anatomy Dissection Manual, kinachomwelekeza mwanafunzi namna ya kupasua mwili wa binadamu na kujifunza sehemu mbalimbali za mwili, hasa kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili kabla ya kuanza mazoezi ya vitendo ya upasuaji.
Pia kuna Essentials of Human Embryology, kinachomwelekeza mwanafunzi kuhusu namna mwili wa binadamu unavyoumbika tumboni kwa muda wa miezi tisa kabla ya mtoto kuzaliwa.
Kitabu cha Histology kinamsaidia mwanafunzi kujifunza namna ya kuchunguza mwili wa binadamu kwa kutumia darubini na kutambua muonekano wa sehemu mbalimbali za mwili, ikiwemo ngozi na mifupa.
Vilevile, kuna Practical Manual on Tooth Morphology, kinachomwelekeza mwanafunzi anayesomea afya ya kinywa na meno kwa undani.
Kitabu kingine ni Postnatal Growth of the Craniofacial Region and the Masticatory Apparatus, ambacho kimelenga kumsaidia mwanafunzi anayebobea katika masomo ya kinywa na meno, hususan kwa watoto.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 25, 2026, jijini Dar es Salaam, mwandishi wa vitabu hivyo, Profesa wa Anatomia wa MUHAS, David Ngassapa, amesema vitabu hivyo vitakuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wa udaktari.
Amesema anatomia ni somo la msingi katika taaluma ya udaktari kwa kuwa ndilo linalomwezesha mwanafunzi kuuelewa mwili wa binadamu, mifumo yake na mabadiliko yanayotokea katika hatua mbalimbali za maisha.
Profesa Ngassapa amesema vitabu hivyo vimeandaliwa kwa lugha rafiki na vimezingatia mfumo wa elimu unaolenga umahiri, tofauti na mfumo wa zamani uliosisitiza zaidi kukariri.
“Mitaala yetu sasa inazingatia umahiri. Huwezi kuwa na mtaala wa umahiri halafu vitabu vinazungumzia kitu kingine. Sisi tumehakikisha vitabu vinaendana moja kwa moja na mfumo wa sasa ili mwanafunzi aelewe na aweze kutumia maarifa yake” amesema Profesa Ngassapa.
Ameongeza kuwa gharama za kuandaa vitabu hivyo zimetolewa na MUHAS, huku akieleza kuwa chuo kina mpango wa kuvitoa vitabu hivyo katika mfumo wa kidijitali ili kuendana na matumizi ya teknolojia katika elimu.
Naye, Kaimu Rasi wa Ndaki ya Tiba wa MUHAS, Profesa Agricola Joachim, amempongeza Profesa Ngassapa kwa juhudi zake za kuandaa vitabu hivyo, akisisitiza kuwa ni jukumu la chuo kufundisha na kufanya tafiti.
Amewahimiza walimu wengine kuandika vitabu vitakavyowasaidia Watanzania, huku akitoa wito kwa wanafunzi na jamii kuvitumia kikamilifu ili kupata elimu inayozingatia umahiri na kuwafanya wawe wataalamu bora zaidi katika sekta ya afya.
MUHAS imeweka alama mpya katika juhudi za kuimarisha elimu ya tiba kwa kuzingatia uhalisia wa mazingira ya wanafunzi na mahitaji ya mfumo wa sasa wa elimu.
