MKURUGENZI wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi amemaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 20 kwa wakazi eneo la C Centre lililopo kata ya Nkuhungu Jiji la Dodoma.
Akizungumza katika kikao cha pamoja kati makundi mawili ya wananchi waliokuwa na misimamo tofauti na timu ya maafisa ardhi wa Halmashauri ya Jiji kujadili namna ya kuwasaidia wananchi wa eneo hilo la C Centre katika ukumbi wa Jiji amesema ipo haja ya serikali kuwasaidia wananchi hao kupata stahiki zao katika eneo hilo lakini wanatakiwa kuwa wakweli na waadilifu.
“Nataka kila mtu atambue kuwa yeye ni mvamizi kwenye eneo hili lakini serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli haiwezi kuwaacha wananchi wake wakataabika hivyo tumeamua kufanya hisani kwa kuhakikisha kila mtu apate kiwanja eneo hilo ili ajenge” Alisema Kunambi
“Endapo mtu mwenye haki ya kupata eneo la C Centre akalikosa kwa sababu yoyote ile halmashauri itajitahidi kumtafutia eneo jingine lakini kwanza tumalize na hawa waliokuwa wakiishi hapo kwa miaka mingi na hawana mbadala wa mahali pengine pa kuishi”. Aliongeza Kunambi.
Kufuatia hatua hiyo makundi yaliyokuwa yakisigana kwa muda mrefu bila kupata suluhu na wengine kushindwa hata kusalimiana wameonyesha furaha yao mbele ya Mkurugenzi wa Jiji na kuahidi kudumisha mshikamano katika eneo hilo.
Baadhi ya wajumbe waliowakilisha wananchi wanaishi katika eneo hilo wamemshukuru Mkurugenzi wa Jiji na kuahidi kusimamia utaratibu waliokubaliana kwa pamoja na kuhakikisha hakuna udanganyifu utakaojitokeza kwenye kuwatambua wananchi wanaotakiwa kupewa viwanja katika eneo hilo.
Naye Mtendaji wa Mtaa wa C Centre wameahidi kusimamia zoezi hilo kwa uaminifu na kuomba ushirikiano kutoka kwa wananchi kuweza kubaini watu wenye nia ovu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Kunambi ameahidi kupima upya eneo hilo ili kukidhi hitaji la wananchi hao na kuhakikisha zoezi hilo linakamilika ndani ya miezi miwili hadi kukamilika kwake.