Na John Bukuku, Dar es Salaam
Ofisi ya Msajili wa Hazina imesema kuwa Mkutano wa Jukwaa la Wakurugenzi wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Kampuni ambazo Serikali ina Hisa Chache (MIF 2026) utafanyika kuanzia Machi 16 hadi 18, 2026 katika Ukumbi wa PAPU, jijini Arusha.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini – Mashirika ya Kibiashara kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bi. Lightness Mauki, amesema mkutano huo wa tatu tangu kuanzishwa kwa jukwaa hilo unatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya Wakurugenzi wa Bodi na Watendaji Wakuu 150 kutoka kampuni 56 ambazo Serikali inamiliki chini ya asilimia 51 ya hisa.
Amesema Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Mbunge).
Kwa mujibu wa Mauki, kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “From Oversight to Foresight: Advancing Agile and Innovative Leadership under Transformation Pressures” inalenga kuhamasisha mabadiliko ya kimkakati katika uongozi wa kampuni, kutoka kwenye ufuatiliaji wa kawaida wa utendaji kwenda kwenye uongozi bunifu unaotazama mbele na kutambua mapema vihatarishi na fursa.
“Tunataka Wakurugenzi wa Bodi na Watendaji Wakuu wawe na mtazamo wa kimkakati unaojibu kwa haraka mabadiliko ya kiuchumi, kiteknolojia na kibiashara yanayoendelea duniani,” amesema Mauki.
Ameeleza kuwa mkutano huo utajadili masuala mbalimbali ikiwemo utawala unaotazama mbele, ubunifu na ushindani endelevu, athari za siasa na uchumi wa kimataifa (geopolitics), usalama wa mitandao (cybersecurity), pamoja na ulinganifu wa mikakati ya taasisi na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akifafanua kuhusu kampuni zenye hisa chache, Mauki amesema ni zile ambazo Serikali inamiliki chini ya asilimia 51 ya hisa, tofauti na Mashirika ya Umma yanayotambuliwa kisheria pale Serikali inapomiliki asilimia 51 au zaidi kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma, Sura ya 257.
Amesema hadi Juni 30, 2025, kulikuwa na taasisi za umma 252 na kampuni zenye hisa chache 56, hivyo kufanya jumla ya taasisi 308 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Kuhusu mafanikio, Mauki amesema thamani ya uwekezaji wa Serikali katika kampuni hizo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 821.51 mwaka 2020 hadi shilingi trilioni 1.94 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 136.
Aidha, mapato ghafi yameongezeka kutoka shilingi trilioni 6.81 hadi trilioni 10.74, huku faida ikiongezeka kutoka trilioni 1.79 hadi trilioni 1.95 katika kipindi hicho. Katika miaka minne iliyopita, kampuni hizo zimechangia takribani shilingi trilioni 3.67 kama kodi ya mapato ya kampuni.
“Gawio kwa Serikali limeongezeka kutoka shilingi bilioni 58.26 hadi bilioni 266.52, sawa na ongezeko la asilimia 357. Hii inaonesha kuwa hatua tulizochukua katika kuimarisha usimamizi, uwakilishi wa Serikali kwenye Bodi na ufuatiliaji wa utendaji zimeleta matokeo chanya,” amesema Mauki.
Ameongeza kuwa kampuni hizo zimeendelea kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi kwa kuongeza ajira, kukuza ujuzi wa Watanzania na kuchangia ukuaji wa sekta muhimu kama benki, madini, nishati, mawasiliano na viwanda.
Mkutano wa MIF 2026 unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha uongozi wa kimkakati katika kampuni ambazo Serikali ina hisa chache, ili kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unaendelea kuleta tija na manufaa ya muda mrefu kwa Taifa.
