NA DENIS MLOWE IRINGA
KATIKA kikao chake cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji Mafinga limeidhinisha rasimu ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 yenye thamani ya Shilingi 38,651,155,000.
Rasimu hiyo iliwasilishwa na Afisa Mipango na Uratibu wa Mji, Peter Ngussa, akimuwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri. Akifafanua, alisema kuwa fedha hizo zimepangwa kutumika kwenye utekelezaji wa majukumu ya maendeleo pamoja na kuboresha huduma kwa wananchi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa maelezo yake, Shilingi 8,884,800,000 zinatarajiwa kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri, ilhali Shilingi 942,454,000 ni ruzuku ya matumizi mengineyo (OC) kutoka serikali kuu. Fedha hizo zinapangwa kuelekezwa kwenye miradi ya kuongeza uwezo wa ukusanyaji mapato, ununuzi wa maeneo mapya ya uwekezaji, uendelezaji wa miradi ya kimkakati na kuboresha huduma za jamii.
Vipaumbele vingine katika bajeti hiyo vinajumuisha kuimarisha usafi na kulinda mazingira ya Mji wa Mafinga, pamoja na kuhakikisha utoaji wa huduma bora unaendelea kuimarika.
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Linda Seleko; Mkurugenzi wa Halmashauri, Fidelica Myovella; Mwenyekiti wa Halmashauri, Regnant Kivinge; Mbunge wa Viti Maalum (Kundi la Vijana), Jasmine Ng’umbi; pamoja na Mbunge wa Mafinga Mjini, Dickson Lutevelle.
Baada ya kupitia hoja mbalimbali, Baraza la Madiwani lilikubali rasimu hiyo na kuahidi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wake ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya na kuendeleza maendeleo ya wakazi wa mji huo.

