NA DENIS MLOWE IRINGA

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Daud Yassin, amesema siku 100 za uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan zimeleta muelekeo mpya wa maendeleo unaoonekana wazi katika sekta mbalimbali nchini Tanzania.

Akizungumza kupitia taarifa aliyochapisha katika mitandao ya kijamii, Yassin alisema hatua na maamuzi yaliyotekelezwa katika kipindi kifupi yamezidi kuongeza matumaini kwa wananchi wa mikoa yote na kujenga uaminifu hususan kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Iringa.

Amesema kuwa ndani ya siku 100, serikali imeendelea kushughulikia changamoto za wananchi kwa kasi, jambo linalothibitisha dhamira ya dhati ya Rais Samia katika kuimarisha ustawi wa taifa.

Yassin alibainisha kuwa miradi ya miundombinu, afya, elimu na uwekezaji imeendelea kupewa kipaumbele, hatua inayowafanya wananchi waone mwanga wa maendeleo unaoleta matumaini ya kweli kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Ameeleza pia kuwa ushirikiano uliopo kati ya serikali na wananchi umeimarika zaidi, kutokana na kiwango kikubwa cha uwazi, usikivu na utatuzi wa changamoto zinazotolewa na mamlaka mbalimbali.

Katika taarifa yake, Yassin alisisitiza kuwa kipindi cha siku 100 kimedhihirisha uwezo mkubwa wa uongozi wa Rais Samia, hususan katika kudumisha amani, utulivu na mshikamano ambao umaendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.

Aidha, alisema kuwa amani iliyopo imeifanya Tanzania kuwa kivutio kwa wawekezaji na jumuiya ya kimataifa, hatua ambayo itachochea fursa zaidi za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Yassin aliendelea kusisitiza kuwa hatua zinazochukuliwa na serikali zimekuwa na tija katika kuboresha huduma muhimu za kijamii, ikiwemo upatikanaji wa maji, nishati, huduma za afya na elimu.

Amesema mafanikio hayo yanaonyesha namna viongozi wote wa serikali wanavyotekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na kujali maslahi ya wananchi.

Mwisho, Yassin alimaliza kwa kuungana na Watanzania wote kumtakia heri Rais Dkt Samia pamoja na viongozi wote katika kuendeleza juhudi za kuiletea Tanzania maendeleo endelevu na ustawi wa taifa.