Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Joseph Rwiza Kashushura,akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Desderius Haule,akifungua kikao Cha Baraza la Madiwani kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo,kulia Makamu Mwenyekiti Alex Nguhi na kushoto Mkurugenzi Mtendaji Joseph Kashushura Rwiza.
………….
Na Mwandishi Wetu, Mbinga
HALMASHAURI ya  Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma,imepanga kukusanya kiasi cha Sh. 57,001,588,000,000 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, sehemu kubwa ya fedha hizo zitatumika kukamilisha  miradi mbalimbali iliyoanzishwa na kutekelezwa kwa nguvu na jitahada za jamii katika vijiji na kata.
Lengo la Halmashauri hiyo ni kuhakikisha jamii inapata huduma bora katika mazingira bora,kuchochea kasi ya maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi na kati ya  fedha hizo Sh. 12,794,512,000.00 za mapato ya ndani ya Halmashauri, Sh bilioni 11,033,647,000.00  kutoka vyanzo visivyolindwa na Sh.bilioni 1,760,850,000.00 kutoka vyanzo vinavyolindwa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Divisheni ya Mipango wa Halmashauri hiyo Christopher Masaaaka,alipokuwa Akiwasilisha  rasmu ya bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Joseph Kashushura.
Masaaka alisema kuwa, Halmashauri imeendelea kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo kwa  mwaka wa fedha 2024/2025 ilikusanya  Sh.bilioni 12.6 sawa na asilimia 106.05% huku makisio yalikuwa Sh.Bilioni 11.9 na  mwaka wa fedha  2025/2026 Halmashauri imefanikiwa kukusanya Bilioni 10.6 sawa na asilimia 99. 40%  na makisio yalikuwa kukusanya shilingi Bilioni 10.69.
Aidha Masaaka alisema,sehemu  ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 imejikita zaidi katika ustawi wa  kijamii na kiuchumi kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya maendeleo ya 2025,mpango mkakati wa Halmashauri pamoja na miongozo mbalimbali ya Serikali, ambapo Sh.31,834,904,000.00  zitatumika kwa ajili  ya mishahara ya watumishi ambazo ni fedha kutoka Serikali kuu.
Kwa mujibu wa Masaaka, sh.1,949,231,000.00 kwa ajili ya matumizi mengineyo ya kawaida kutoka Serikali kuu na Sh.10,432,941,000.00 fedha kutoka Serikali kuu  ambazo zitatumika kutekeleza miradi ya mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri hiyo.
Alisema, katika bajeti hiyo miongoni mwa vipaumbele ni matumizi ya TEHAMA ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji,kuboresha huduma za kijamii,kuendeleza miundombinu ikiwemo kukamilisha miradi viporo  katika sekta ya afya,elimu na utawala bora na usimamizi thabiti wa fedha za umma zinazotokana na mapato ya ndani,ruzuku ya Serikali kuu na michango wa wadau wengine wa maendeleo.
Alitaja mpango mwingine utakaotekelezwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ni kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo ya vijijini kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara  za mijinI na vijijini(TARURA) ambapo Halmashauri imetenga   bajeti ya matengenezo na uendeshaji wa mtambo wake unaoweza kusaidia kuchonga barabara na bajeti ya matengenezo ya barabara zake.
Pia alisema,wamejipanga kuhakikisha wanaendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuimarisha vilivyopo ambapo itawezesha ongezeko la asilimia 16 ya makisio ya Sh.12,794,512,000.00 ambayo yamewekwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027  kutoka Sh.10,693,923,000.00 ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Masaaka alieleza kuwa, vyanzo vipya vilivyobuniwa  na miradi ya kimkakati ni uimarishaji wa eneo la uwekezaji la Ngembambili kwa kujenga soko la mazao ya nafaka na kutwaa maeneo ya ardhi kwa ajili ya kuendeleza eneo hilo maalum  kwa ajili ya shughuli za viwanda,maghala na biashara.
Masaaka  ameongeza kuwa  ili kuendelea kuboresha ukusanyaji wa mapato  Halmashauri imebuni vyanzo vipya vya mapato kwa kuanzisha miradi ya kimkakati ikiwemo kitega uchumi cha Mbinga DC Mall, Mbinga DC Executive Villa, Mradi wa Viwanja vya biashara na Maghala ya nafaka uliopo Ngembambili Kata ya Mkako. Pamoja na kuanzisha shamba la kahawa lenye ukubwa wa Ekari 100 lililopo kijiji cha Kizota.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Desderius Haule,amempongeza Mkurugenzi Mtendaji  Joseph Kashushura na watumishi kwa ukusanyaji wa mapato na usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo hususani ya kimkakati ambayo imewezesha Halmashauri kuendelea kuwa kinara wa ukusanyaji mapato ya ndani katika Mkoa wa Ruvuma kwa miaka 6 mfululizo,kusimamia ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa Miradi ya maendeleo.
Diwani wa Kata ya Ukata Evelin Mwitumba, amesisitiza kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo uendelee kwa kasi ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za kijamii katika mazingira bora.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Kisare Makori,amewataka watumishi wa Serikali mkoani humo kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayotolewa na serikali ili kuleta tija na maendeleo endelevu.
Makori, amewaasa watumishi kufanya kazi kwa uwajibikaji, nidhamu, weledi na kuacha urasimu,kuwajibika kwa nafasi zao ili kuweka msingi wa kulifanya Taifa kupata maendeleo kulingana naDira ya Taifa ya 2050 huku akibainisha kuwa Wilaya ya Mbinga  kuna fursa kubwa za kufikia malengo ya Dira hiyo kutokana na rasilimali mbalimbali.
“Nimefuatilia nimeona mpaka sasa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 mmefanikiwa kukusanya Bilioni 10.6 sawa na asilimia 99. 40% ambayo  makisio ilikuwa kukusanya shilingi Bilioni 10.69. Hii ni hatua nzuri. Niwapongeze sana Mbinga DC.  Hamjawahi kuniangusha.” alisema Makori.