Mwamvua Mwinyi, Pwani
Februari 17, 2026
Serikali kupitia– TAMISEMI imeanza utekelezaji wa mfumo mpya wa tovuti ikiambatana na mafunzo maalum kwa Maofisa Habari na TEHAMA nchini, hatua inayolenga kuondoa changamoto zilizokuwepo awali na kuimarisha uwajibikaji, uwazi na nidhamu ya kazi katika matumizi ya mifumo ya kidijitali.
Mpango huo unakusudia kurahisisha na kuboresha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi kwa wakati, baada ya kubainika kuwa tovuti za awali zilikuwa na changamoto za kiufundi zilizochelewesha uchapishaji wa maudhui na kupunguza ufanisi wa mawasiliano kati ya Serikali na jamii.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tano ya usimamizi na uendeshaji wa tovuti mpya kwa Maofisa Habari na TEHAMA wa Mkoa wa Pwani na Halmashauri zake, Ofisa TEHAMA kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Aloyce Mkomagi, alisema mafunzo hayo yatanufaisha mikoa yote 26 na Halmashauri 184 nchini.
Alieleza baada ya mafunzo hayo, washiriki wanatarajiwa kuwa na uwezo wa kusimamia na kuendesha tovuti mpya kwa ufanisi .
“Mafunzo haya yatatolewa nchi nzima,leo februari 17,2026 tumeanza na Mkoa wa Pwani,” alisema Mkomagi.
Kwa upande wake, Kusirye Ukio, akimwakilisha Ofisa Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, alieleza maudhui yasiyo sahihi huathiri uaminifu wa taasisi, huku mifumo isiyo salama ikiweka taarifa za Serikali katika hatari.
“Mafunzo haya yanapaswa kuonekana kama sehemu ya kuimarisha utamaduni wa uwajibikaji, weledi na nidhamu ya kazi katika matumizi ya mifumo ya kidijitali,” alisisitiza Ukio.
Aliongeza kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa TEHAMA katika kuharakisha utoaji wa huduma, kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kujenga uchumi wa kidijitali.
Ofisa Habari wa Mkoa wa Pwani, Zabron Bugingo, alisema matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ni wajibu wa kiutendaji unaohitajika ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia duniani.
Alisema mafunzo hayo yatakuwa daraja la mawasiliano sahihi kati ya Serikali na wananchi.
Naye Ofisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Ruth Msechu, aliishukuru Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo akisema maboresho yaliyofanyika yatawasaidia kupandisha maudhui kwa urahisi na kwa muda mfupi.
Ofisa TEHAMA wa Kisarawe, Nsanganiye John Bilinzozi, alielezea tovuti zilizokuwa zikitumika tangu mwaka 2017 zilikuwa zikichukua muda mrefu kupandisha maudhui, hali iliyokuwa ikiathiri upatikanaji wa taarifa kwa wananchi.

