KATIKA juhudi za kuboresha huduma ya maji na kuimarisha mazingira ya kujifunzia, Bodi ya Maji Bonde la Rufiji imetekeleza mradi wa maji safi katika Shule ya Msingi Jamhuri iliyopo Kijiji cha Ilongo, wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya kupitia Mradi wa Kuimarisha Mbinu za Asili za Usimamizi wa Vyanzo vya Maji na Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (NBS–USANGU).Mradi huo umefadhiliwa na Serikali ya Japani kupitia World Bank, na umezinduliwa rasmi na mwakilishi wa Balozi wa Japani nchini. Akizungumza wakati wa uzinduzi, mwakilishi huyo amepongeza kasi ya utekelezaji wa mradi na kueleza kuwa ushirikiano kati ya Japani na Tanzania unaendelea kuleta matokeo chanya, hasa katika sekta ya maji na uhifadhi wa mazingira.
Kwa miaka mingi, wanafunzi wa Shule ya Msingi Jamhuri walilazimika kutembea zaidi ya kilomita tatu kutafuta maji hali iliyosababisha uchelewaji wa masomo na kuwachokesha kabla ya vipindi kuanza. Kupitia mradi huu, kisima kirefu kimechimbwa, miundombinu ya usambazaji maji imejengwa na huduma hiyo sasa imefika shuleni na kwa wakazi wa maeneo ya jirani.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Jenifer Sanga, amesema upatikanaji wa maji umeleta unafuu mkubwa kwa mazingira ya masomo:
“Hii ni neema kwa shule na wanafunzi wetu. Muda uliokuwa unapotea kutafuta maji sasa utatumika kusoma.”
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilongo, Benjamini Mwakalonge, amesema mradi huo umeondoa changamoto kubwa iliyowakabili wakazi kwa muda mrefu:
“Sasa jamii nzima inanufaika. Haya maji si ya shule peke yake bali ya wakazi wote wanaoishi karibu na eneo hili.”
Akizungumza kuhusu umuhimu wa mradi huo, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, Mhandisi David Munkyala, amesema mradi wa NBS–USANGU ni sehemu ya mkakati wa bodi kuhakikisha rasilimali za maji zinalindwa na kutumiwa kwa tija pamoja na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Lengo letu ni kuhakikisha tunawafikia wananchi kwa njia endelevu na rafiki kwa mazingira.”
Msimamizi wa mradi kutoka World Bank, Nicholas Soikan, ameihakikishia jamii kuwa benki hiyo itaendelea kuunga mkono miradi inayolenga kuboresha huduma muhimu kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mratibu wa mradi kutoka bodi hiyo, David Muginya, amesema ushirikishwaji wa jamii umechangia kufanikisha utekelezaji:
“Tumeshirikiana na viongozi wa kijiji na uongozi wa shule kuhakikisha mradi unakuwa mali ya jamii na unadumu kwa muda mrefu.

