Na Happy Lazaro, Arusha
Serikali ya Tanzania imeweka mkazo mkubwa katika ujenzi na matengenezo ya barabara za mijini na vijijini, hatua inayolenga kuboresha usafirishaji, kukuza biashara na kuimarisha uchumi wa Taifa.
Uwekezaji huu unaonesha dhamira ya kudumisha maendeleo endelevu na kurahisisha maisha ya wananchi katika kila kona ya nchi.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara Tanzania, Mhandisi Rashid Kalimbaga, alichaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Mifuko ya Matengenezo ya Barabara Afrika (ARMFA), akichukua nafasi ya Essaie Aubin wa Cameroon aliyemaliza muda wake. Hatua hii inapanua ushawishi wa Tanzania katika usimamizi wa miundombinu ya barabara barani Afrika na inaashiria kuendelea kushirikiana kwa karibu na nchi za jirani.
Uongozi wa Mhandisi Kalimbaga unatarajiwa kuimarisha mshikamano wa ki-Afrika katika kuhakikisha matengenezo bora, ubunifu katika barabara, na kuendeleza miradi ya kimkakati inayounganisha miji, vijiji na masoko.
“Hii pia ni fursa ya kuunda mtandao thabiti wa barabara utakaoboresha usafirishaji wa bidhaa na huduma ndani ya nchi na kwingineko.”amesema.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Abdallah Ulega, amesema uwekezaji huu ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuhakikisha usafirishaji ni rahisi, biashara inakua, na uchumi wa taifa unaimarika.
Amesisitiza kwamba kila mradi wa barabara una lengo la kuleta tija kwa wananchi na kuunda mazingira yanayofaa kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo.
Kwa wananchi, miradi hii inatoa fursa kubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kuimarishwa kwa barabara kunarahisisha usafirishaji wa bidhaa, kupunguza gharama za usafirishaji, na kuongeza ufanisi wa biashara za ndani.
Ni hatua inayowakilisha kielelezo cha maendeleo endelevu na kipaumbele cha Serikali katika kuinua maisha ya wananchi wa Tanzania.

