Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma

 

………..

Na John Bukuku, Dar es Salaam

Hatua ya watengeneza maudhui mtandaoni kutumia fursa ya punguzo la bei ya usajili kujisajili rasmi ni jambo la msingi linaloweza kuwatenga na makosa ya kufanya kazi bila kufuata matakwa ya kisheria. Kwa kipindi kirefu, baadhi ya wabunifu walikuwa wakiendesha shughuli zao bila leseni rasmi, hali iliyokuwa ikiibua hoja za kisheria na kitaaluma kuhusu uhalali wa kazi zao. Sasa mazingira yamebadilika, na kilichobaki ni wao kuchukua hatua stahiki ya kujisajili.

Kufuatia malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa mablogger na watengenezaji wa maudhui mtandaoni kuhusu gharama kubwa za leseni, Serikali imechukua hatua ya kushusha ada hiyo ili kuwawezesha wabunifu wengi zaidi kushiriki rasmi katika sekta ya kidijitali.

Kazi inaendelea

 

Kwa muda mrefu, watengenezaji wa maudhui walikuwa wakilalamikia kiwango cha ada ya leseni kilichofikia shilingi milioni 1, na baadaye kikashuka na kifikia laki 5 wakieleza kuwa ni kikubwa na kinawaumiza kiuchumi, hususan kwa wabunifu chipukizi na wanaojitegemea. Walisisitiza kuwa gharama za usajili na ada kuwa juu zilikuwa kikwazo kwa ukuaji wa tasnia ya ubunifu wa maudhui ya mtandaoni pamoja na kupunguza hamasa ya kujisajili kisheria.

Hatua ya kupunguza ada imetangazwa rasmi na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Watangazaji uliofanyika jijini Dodoma Februari 12–13, 2026.

Katika tangazo hilo, Naibu Waziri alisema Serikali imezingatia kilio cha wadau na kuamua kushusha ada ya leseni kutoka shilingi milioni 1 hadi shilingi 50,000. Aidha, ada ya maombi imewekwa katika kiwango cha shilingi 10,000, hivyo kufanya jumla ya gharama kwa mwombaji mpya kuwa shilingi 60,000.

Alieleza kuwa uamuzi huo unalenga kukuza sekta ya ubunifu wa kidijitali, kuongeza ajira kwa vijana, pamoja na kurahisisha usajili rasmi wa watengenezaji wa maudhui ili waweze kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria na kanuni za nchi.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Mwanasheria Patrick Kipangula

 

Hata hivyo, pamoja na punguzo hilo la ada, changamoto nyingine inayowakabili vijana wengi watengeneza maudhui ya kihabari katika sekta ya kidijitali ni kuhakikisha wanakidhi vigezo vya kitaaluma na kiuandishi vilivyowekwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Tanzania (JAB).

Akiwasilisha mada katika mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Mwanasheria Patrick Kipangula, aliwasisitiza wanahabari na watengeneza maudhui kujikita katika kujiendeleza kitaaluma ili kukidhi matakwa ya kisheria ya taaluma ya uandishi wa habari. Alieleza kuwa ni muhimu kufikia angalau kiwango cha cheti cha Astashahada (Diploma) katika fani ya uandishi wa habari au mawasiliano ili kuidhinishwa rasmi na Bodi na kupewa leseni ya uandishi wa habari.

Kwa mujibu wa Kipangula, msisitizo huo unalenga kulinda weledi wa taaluma, kuhakikisha ubora wa maudhui ya habari yanayochapishwa mtandaoni pamoja na kujenga uwajibikaji kwa jamii.

Dkt. Jabiri Kuwe Bakari. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA

 

Sambamba na hilo, uamuzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kushusha gharama za leseni unapaswa kutazamwa kama dirisha jipya la kuwavuta rasmi wale wote waliokuwa wakifanya kazi bila kujisajili kwa sababu ya gharama za usajili na ada kuwa juu. Sasa ni wakati wao kujisajili ili wafanye kazi zao kihalali bila kukiuka sheria na kanuni zinazosimamia sekta ya maudhui mtandaoni.

Hatua hiyo pia inatarajiwa kuongeza uwajibikaji, kulinda haki za watumiaji wa habari, na kuweka mazingira rafiki ya ushindani sawa miongoni mwa wabunifu wa maudhui ya kidijitali.

Kwa mtazamo mpana, punguzo la ada linafungua ukurasa mpya wa mageuzi ya sekta ya maudhui mtandaoni — lakini mafanikio yake yatategemea utayari wa wahusika kutumia fursa hiyo kujisajili, kujiendeleza kitaaluma, na kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria, maadili na viwango vya taaluma ya habari nchini.

Mwisho, ni vyema kuishukuru Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kuchukua hatua hiyo muhimu ya kuwatua mzigo wa gharama za usajili wanamitandao. Punguzo hili siyo tu limeondoa kikwazo kikubwa bali pia limefungua milango ya fursa kwa wabunifu wengi zaidi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa kidijitali. Sasa ni wakati wa wanamitandao kujisajili, kufanya kazi kwa weledi na uhalali, na kwa pamoja “tukapige kazi” kulijenga taifa.