NA DENIS MLOWE IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhil Ngajilo, ameendelea kutekeleza ahadi aliyoitoa kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kutoa mafunzo maalum ya ujasiriamali kwa wakazi wa jimbo hilo.
Wajasiriamali 300 kutoka Manispaa ya Iringa wamenufaika na mafunzo hayo ya siku sita yaliyojikita katika kuongeza ujuzi wa kuendesha biashara kwa tija.
Mafunzo hayo yameratibiwa na Ofisi ya Mbunge kwa lengo la kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati kupata mbinu za kisasa za kukuza mitaji, kuongeza mauzo na kuimarisha usimamizi wa biashara.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mbunge, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Tumaini Msowoya, aliwataka washiriki kutumia teknolojia kama nyenzo ya ushindani katika biashara za kisasa. Alieleza kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali ni fursa kubwa ya kupanua masoko na kuongeza wigo wa wateja ndani na nje ya Mkoa wa Iringa.
Katibu wa Mbunge wa Iringa Mjini, Yahaya Mpelembwa, alibainisha kuwa mafunzo hayo yamekusudiwa kuwa chachu ya mafanikio ya biashara kwa kuwapa washiriki maarifa katika maeneo ya masoko, usimamizi wa fedha, huduma kwa wateja na mbinu za kuongeza mitaji.
Kwa upande mwingine, Meneja wa Star Entrepreneur General kutoka Mkoa wa Morogoro, Issa Bashir, aliushukuru uongozi wa Mbunge kwa kuwapa wajasiriamali wa Iringa fursa ya kupata mafunzo ya vitendo katika sekta mbalimbali ikiwemo ufugaji wa kuku, utengenezaji wa keki, kilimo cha kibiashara, ujasiriamali wa viwandani na mbinu za kutafuta masoko.
Mafunzo hayo yameatajwa kuwa hatua muhimu ya utekelezaji wa ahadi ya Ngajilo ya kuwainua wajasiriamali wa eneo hilo, huku yakitarajiwa kuongeza thamani ya bidhaa, kupanua biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Manispaa ya Iringa na mkoa mzima.