Na Silivia Amandius
Bukoba.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba limepitisha rasimu ya bajeti ya shilingi bilioni 51.9 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo na matumizi ya kawaida katika wilaya hiyo.
Bajeti hiyo imeidhinishwa katika mkutano wa pili wa Baraza la Madiwani uliofanyika kwa ajili ya mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 pamoja na mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2025/2026.
Akiwasilisha bajeti hiyo mbele ya Baraza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri, Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu, Bi. Rahel Mbuta, alisema Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba inakadiria kukusanya, kupokea na kutumia jumla ya shilingi bilioni 51.9 kwa ajili ya kuimarisha huduma za jamii na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Alisema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 33.7 zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, shilingi bilioni 4.9 zinatarajiwa kukusanywa kupitia mapato ya ndani, shilingi bilioni 1.8 zimetengwa kwa matumizi mengineyo ya uendeshaji, huku shilingi bilioni 11.2 zikitengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Bi. Rahel alieleza kuwa bajeti hiyo imezingatia vipaumbele muhimu ikiwemo kuimarisha mikakati ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuongeza uwezo wa Halmashauri kujitegemea kutoka asilimia 8.5 hadi kufikia asilimia 10.5 ifikapo Juni 2027, pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.
Aidha alisema Halmashauri imejipanga kupambana na changamoto za kiafya na kijamii kwa kupunguza kiwango cha udumavu wa watoto chini ya miaka mitano, kupunguza maambukizi ya VVU na UKIMWI kutoka asilimia 3 hadi 2.5 ifikapo mwaka wa fedha 2026/2027, pamoja na kuimarisha usalama wa chakula na lishe kwa wananchi.
Baadhi ya madiwani akiwemo Mheshimiwa Jasson Lwankomezi, Diwani wa Kata ya Kaibanja, wameunga mkono kupitishwa kwa bajeti hiyo na kuipongeza menejimenti ya Halmashauri chini ya Mkurugenzi Bi. Fatma Hussen pamoja na watumishi wake kwa maandalizi ya bajeti hiyo.
Madiwani wamewataka watumishi wa Halmashauri kuhakikisha fedha hizo zinasimamiwa kwa uwazi na ufanisi ili ziweze kutumika ipasavyo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan katika sekta za kilimo, uvuvi, ufugaji, afya na elimu, kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi wa Wilaya ya Bukoba.

