Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Beno Malisa amelipongeza Jeshi la Polisi Mbeya kwa utendaji kazi mzuri hasa katika kukabiliana na kesi za ukatili wa kijinsia ikiwemo kubaka na kulawiti.

Amezungumza hayo katika sherehe za Maadhimisho ya siku ya familia ya Polisi Mbeya iliyofanyika Februari 14, 2026 katika uwanja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoani humo huku zikipambwa na gwaride rasmi lililoandaliwa na vikosi mbalimbali vya Polisi Mbeya.

Mhe Malisa mbali na kupongeza jitihada za Jeshi la Polisi hususani kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto katika kukabiliana na kesi za ukatili, pia ameitaka jamii kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za vitendo vya ukatili na kuacha kumalizana kienyeji ili kutokomeza uhalifu huo.

Sambamba na hayo, Mhe Malisa aliwatunuku vyeti vya sifa Askari Polisi 15 kutoka vitengo mbalimbali kwa utendaji kazi mzuri zaidi kwa kipindi cha mwaka 2025 huku Askari kutoka Dawati la Jinsia na Watoto wakiibuka vinara katika tuzo hizo.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga ameiomba jamii kutoficha matukio ya ukatili ikiwemo ubakaji na ulawiti na badala yake watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa.

Miongoni mwa Askari waliotunukiwa tuzo hizo kwa niaba ya Askari wengine Sajenti Twitike Mwakalebela na Polisi Konstebo Raymond Joseph wamemshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga kwa kuona jitihada zao na kutambua utendaji wao huku wakiahidi kuendelea kushirikiana na Askari wenzao, idara nyingine na Wananchi ili kubaini na kuzuia uhalifu katika jamii.

Siku Maalum ya Familia ya Polisi hufanyika kila mwaka ambapo huambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo zoezi la upandaji miti, uchangiaji wa damu salama, kutoa msaada kwa makundi yenye mahitaji, michezo mbalimbali na kuhitimishwa kwa sherehe ya utoaji wa tuzo na zawadi kwa Askari waliofanya vizuri zaidi katika utendaji kazi za Polisi.