Na. Mwandishi Wetu – Dodoma

Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, amesema taasisi hiyo itaendelea kusimamia kwa nguvu zote uhifadhi wa misitu na rasilimali za nyuki kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi, huku ikiimarisha matumizi ya teknolojia ya kisasa kukabiliana na uharibifu wa misitu.

Akieleza majukumu ya msingi ya TFS, leo Februari 13, 2026 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wakala hiyo iliyofanyika Jijini Dodoma, Prof. Silayo amesema taasisi hiyo inawajibika kuhifadhi na kusimamia misitu ya hifadhi iliyo chini ya Serikali Kuu, kulinda rasilimali za nyuki, kuendeleza mashamba ya miti kwa matumizi ya viwanda na jamii, pamoja na kusimamia uvunaji endelevu wa mazao ya misitu.

Amesisitiza kuwa katika utekelezaji wa majukumu hayo, TFS itaweka mkazo katika kulinda bioanuwai na mifumo ikolojia, kuhifadhi vyanzo vya maji vinavyotegemea misitu, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuzuia ukataji haramu pamoja na uvamizi wa misitu.

Amesema taasisi hiyo tayari imeanza kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ufuatiliaji wa rasilimali misitu, ikiwemo matumizi ya satelaiti na ndege nyuki (drones) kubaini uharibifu kwa wakati. Aidha, mifumo ya intelijensia na upelelezi imeboreshwa ili kudhibiti makosa ya misitu kabla hayajasababisha athari kubwa.

Prof. Silayo ameongeza kuwa TFS pia inaendelea kuimarisha nidhamu na weledi miongoni mwa askari wa uhifadhi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa sheria. Sambamba na hilo, amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi wanaozunguka misitu, akieleza kuwa uhifadhi endelevu hauwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa jamii.

Amebainisha kuwa katika kukuza uchumi na kupunguza utegemezi unaochochea uharibifu wa misitu, TFS itaendelea kuhamasisha ufugaji wa nyuki kama chanzo mbadala cha kipato, kuongeza thamani ya mazao ya misitu na nyuki, pamoja na kushirikiana na sekta binafsi.