Na John Bukuku – Dodoma
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA Dkt. Jones A. Kilimbe amesema utangazaji si biashara tu bali ni huduma ya kijamii yenye wajibu mkubwa kwa taifa, akisisitiza kuwa vyombo vya utangazaji vina nguvu ya kuelimisha, kubadilisha mitazamo na kuhamasisha maendeleo hivyo vinapaswa kutumia nguvu hiyo kwa manufaa ya umma.
Amesema hayo Februari 13, 2026 jijini Dodoma wakati akizungumza katika hafla ya kufunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Watangazaji uliofanyika kwenye Ukumbi wa New Generation Hall kwa niaba ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma.
Amebainisha kuwa mijadala ya mkutano huo imejikita katika matumizi ya teknolojia za TEHAMA za kisasa, ubora wa maudhui, uendelevu wa biashara za utangazaji, maadili ya kitaaluma pamoja na wajibu wa vyombo vya habari katika kujenga jamii yenye mshikamano hususan kwa wananchi wa vijijini.
Dkt. Kilimbe ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutambua na kuthamini mchango wa sekta ya utangazaji katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni, akisisitiza kuwa maazimio na mapendekezo yaliyotolewa yanapaswa kutekelezwa kwa vitendo kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo sambamba na kuimarisha weledi, uwajibikaji na maadili ya taaluma.
Amesema katika zama za mapinduzi ya kidijiti, wanahabari wanapaswa kuwa wabunifu zaidi katika uandaaji na urushaji wa maudhui kupitia majukwaa ya kidijiti na mitandao ya kijamii ili kuyafikia makundi mapya ya hadhira hususan vijana bila kuathiri misingi ya taaluma.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kufanya tafiti za habari na hadhira mara kwa mara akieleza kuwa tafiti ni dira ya maamuzi sahihi ya kimaudhui na kibiashara na husaidia kubaini mahitaji halisi ya walaji wa maudhui na kuongeza ubora, ufanisi na ushindani.
Pia ameeleza kuwa maudhui yanapaswa kumlea mtoto wa Kitanzania katika maadili mema na kuepuka yale yanayoweza kuharibu maadili, afya ya akili au mustakabali wao, akisisitiza kuwa maudhui yana athari kubwa kwa jamii.
Ameongeza kuwa hatua za awali zinaendelea katika utekelezaji wa mapendekezo yaliyotokana na utafiti wa kina wa sekta ya utangazaji uliofanywa na mshauri mwelekezi Dotto, ulioweka mezani taswira halisi ya maendeleo na changamoto za tasnia hiyo.

