Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema ipo pamoja na vijana katika kubuni mbinu mbalimbali ili kuzifikia fursa za ajira nchini
Mkurugenzi wa Maendeleo Idara ya Vijana Zanzibar Shaibu Muhammed Ibrahim ameyasema hayo katika Ukumbi wa Skuli a Secondary Tumekuja Wilaya ya Mjini wakati akifungua Semina Elekezi kwa Kamati ya kusimamia Uchaguzi wa Baraza la Vijana Ngazi ya Wilaya na taifa

Amefahamisha kuwa  Sera ya Maendeleo ya Vijana ni Kuwepo kwa Baraza la Vijana ili kufanikisha ndoto zao katika kuzifikia fursa mbalimbali

Amesema kuwa maisha ya vijana yapo  mikononi mwa Kamati ya Kusimamia Uchaguzi wa Baraza hilo hivyo ni vyema kuhakikisha wanachukua jitihada mbalimbali ili kuepusha mifarakano kwa vijana hao

Aidha ameitaka Kamati hiyo kuhakikisha inapiga vita ukabila ,ukanda  na siasa kwani havitosaida katika kupata viongozi bora, hivyo ni vyema kufanya Uchaguzi wa haki ,Amani na utulivu
“Lengo la Baraza la Vijana ni kuwaunganisha vijana na kuwa wamoja” alisisitiza Mkurugenzi
Aidha amempongeza Waziri wa Wizara hiyo kwa kuteua timu nzuri ambayo itawasaidia vijana katika kufanikisha matarajio na lengo la Serikali
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Baraza la Vijana Ngazi ya Wilaya na taifa Ame Haji Vuai amesema kuwa Kamati ipo tayari kushirikiana na Baraza kwa kufanya uchaguzi wa haki huru na salama
Nao vijana waliyopatiwa semina hiyo wameahidi kuyafanyia kazi kwa mashirikiano na kufuata maelekezo waliyopewa ili kufanikisha lengo linalotarajiwa.
Semina hiyo ni muendelezo kufuatia Kuwepo kwa Uchaguzi wa Baraza la Vijana kwa Ngazi ya Shehia,Wilaya na Taifa unayotarajiwa kufanyika Machi mwezi ujao.