Wananchi wa Halmashauri ya Mji Ifakara wameendelea kunufaika na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unaotekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ( NHIF) ikiwa ni ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo leo alhamisi tarehe 12 Februari 2026 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Bi. Pilly Kitwana ameongoza zoezi la kugawa kadi 144 za Bima ya Afya katika Kata ya Kiberege. Kadi hizo zinatolewa kwa makundi ya wazee, wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, watu wenye mahitaji maalumu pamoja na Kaya zenye hali duni.
Aidha ,Bi. Kitwana alimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa kadi hizo za Bima ya Afya kwa Wote hatua iliyowaletea faraja wananchi wengi.
” Gharama za Bima ya Afya kwa Kundi hili zinalipiwa na Serikali ikiwa ni Utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Wananchi wote hususani makundi yenye uhitaji maalum wanapata huduma Bora za Afya bila kikwazo cha Fedha” . Alieleza Bi. Kitwana
Aliongeza kuwa utekelezaji wa mpango huo umeleta tabasamu kwa wananchi, hususan wale wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za bima ya afya.
Kwa upande wake, Mratibu wa TASAF Ifakara Mji Bi. Brigita Haule, alisema Bima hizo ni muhimu sana kwani zitawasaidia wananchi wanapopatwa na changamoto za kiafya kuhudumiwa bila vikwazo na kwamba ugawaji wa kadi unaendelea katika kata zote 19 za Halmashauri ya Mji Ifakara kwa Awamu ya kwanza iliyoanza tarehe 7 /2/2026 Hadi tarehe 21/2/2026 huku juhudi zikifanyika kuhakikisha walengwa wote wanafikiwa.
Mmoja wa wanufaika Bi. Safina Ninje, alimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia Kadi za bima ya afya , akisema kuwa ni msaada mkubwa na unawapa uhakika wa matibabu.
Jumla ya wanufaika 4,161 katika Halmashauri ya Mji Ifakara wanatarajiwa kufikiwa na kupatiwa kadi za Bima ya Afya Bure. Mpango huo unaendelea kutekelezwa kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za Afya na kuinua Ustawi wa Wananchi.
