NA DENIS MLOWE, MAFINGA 

MKUU wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Selekwa, amewapongeza madiwani wote wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga kwa kuaminiwa na wananchi na kupewa dhamana ya kuwatumikia kwa kipindi cha miaka mitano ijayo huku akitoa wito kwa viongozi hao kuweka mbele maslahi ya wananchi na kuhakikisha maendeleo ya mji yanaendelezwa kwa mipango thabiti.

Akizungumza mbele ya baraza la madiwani, Dkt. Selekwa aliwataka kutumia nafasi zao kama watawaliwa wa wananchi kwa uwajibikaji mkubwa, akisisitiza kuwa ofisi yake iko wazi wakati wowote kwa ajili ya kupokea hoja au changamoto zozote zinazohitaji ushirikiano na serikali.

“Ofisi yangu ipo wazi, karibuni wakati wowote kujadili mambo yanayohusu kata zenu au halmashauri kwa ujumla. Sisi sote ni sehemu ya serikali; tukishirikiana tutafika mbali,” alisema.

Katika hotuba yake ya Salamu za Serikali, Dkt. Selekwa alieleza kuwa kasi ya ukuaji wa Mji wa Mafinga inahitaji uangalizi wa karibu, hasa katika mipango ya ardhi na aliwataka madiwani na wataalam kuhakikisha mji unapangwa mapema ili kuepusha athari za kijamii na kimazingira zitakazoweza kujitokeza baadaye.

“Tusipo panga mji mapema, changamoto zitakuja kuwa kubwa. Leo watu wanajenga popote wanapotaka. Kesho tukipata mafuriko, lawama zitarudi kwetu,” alionya.

Amempongeza pia Katibu Tawala wa Wilaya kwa kusimamia kikamilifu taratibu za ujenzi na kuzuia majengo yaliyojengwa katika maeneo yasiyostahili.

Dkt. Selekwa amelitaka Baraza la Madiwani kuipa kipaumbele Kamati ya Mipango Miji na Mazingira kuhakikisha upangaji wa mji unafanyika kwa kasi na ufanisi mkubwa, akisema kuwa serikali haitaki kusubiri mpaka matatizo yatokee ndipo ichukue hatua.

Mkuu huyo wa Wilaya alisisitiza kuwa mafanikio au changamoto za Halmashauri ya Mafinga ni jukumu la kila kiongozi, akiwemo diwani, mtendaji na watalaam wote.

“Halmashauri hii ni yenu. Kuipeleka mbele au kuirudisha nyuma ni juu yenu. Sisi wataalam tunaweza kutoka, lakini ninyi mtabaki. Basi tumieni nafasi hii vizuri kwa maslahi ya wananchi,” alisisitiza.

Katika eneo la kilimo, Dkt. Selekwa aliwataka madiwani kufatilia kwa karibu upatikanaji wa mbolea kwenye kata zao ili kuwaepusha wananchi na ucheleweshaji unaoweza kuathiri uzalishaji. Alisema pamoja na juhudi za wataalamu, madiwani wanabaki kuwa kiunganishi muhimu kati ya wananchi na Serikali.

Dkt. Selekwa alisifu kazi iliyofanywa na baraza lililopita katika kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni, akisisitiza kuwa suala hilo linapaswa kuendelezwa kwa asilimia 100.

Aidha, aligusia changamoto ya watoto wenye utapiamlo katika baadhi ya kata na kuwataka madiwani kufuatilia sababu zinazosababisha hali hiyo ili kusaidia kutatua tatizo hilo kikamilifu, huku akitaja mfano wa baadhi ya familia zenye changamoto kubwa katika malezi.

Katika hitimisho, aliwataka madiwani kuendelea kuisimamia serikali kwa weledi na kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa haraka na kwa maslahi ya wananchi wote wa Mafinga.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Regnant Kivinge amesema uongozi wa wilaya umeendelea kuwa chachu ya utulivu na mwenendo mzuri wa shughuli za utawala katika mji huo.

Katika hotuba yake, Mwenyekiti huyo amewapongeza madiwani wapya kwa kuaminiwa na wananchi katika kata zao, akisisitiza kuwa ushindi wao ni dhamana kubwa ya kuiwakilisha jamii katika masuala ya maendeleo.

Pia amepongeza mazingira salama na utulivu yaliyowezesha kufanyika kwa uchaguzi na kuundwa upya kwa baraza la halmashauri bila changamoto.

Akimuelekea Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti amesisitiza mchango mkubwa wa kamati ya ulinzi na usalama katika kuhakikisha shughuli za halmashauri zinaenda kwa mpangilio hata kipindi ambacho baraza lilivunjwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria. 

Amesema ufuatiliaji na maelekezo ya DC yamekuwa nguzo muhimu katika kuimarisha utendaji wa menejimenti ya halmashauri.

Aidha, amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri na timu yake kwa kuendeleza kazi kwa ufanisi mkubwa baada ya mabaraza kuvunjwa, huku akibainisha kuwa juhudi za pamoja kati ya menejimenti na viongozi wa wilaya zimeiwezesha Halmashauri ya Mji Mafinga kuendelea kusonga mbele.