Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya leo, 10 Februari 2026, imepokea ugeni mkubwa wa viongozi wa ngazi ya juu wa Shirika la Walter Reed Army Institute of Research (WRAIR) kutoka nchini Marekani ukiongozwa na Colonel (COL) Brianna Perata, ambaye ni Kamanda wa WRAIR/DOW, pamoja na maofisa wengine alioambatana nao ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya nchini Tanzania.
Ujumbe huo umekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Hospitali chini ya Dkt. Godlove Mbwanji Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, lengo kuu likiwa ni kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika masuala mbalimbali ya afya, utafiti, na maendeleo ya huduma za afya kwa ujumla.
Kwa upande wa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili Dkt. Mbwanji ameeleza kuwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya itaendelea kushirikiana na Marekani kupitia programu mbalimbali zilizo chini ya mpango wa PEPFAR zinazohusisha mkoa wa Mbeya na mikoa mingine ya nyanda za juu kusini mwa Tanzania ikiwa ni pamoja na Rukwa, Katavi na Songwe ambapo kupitia programu hizi huduma mbalimbali za afya zimeimarishwa, hasa zile zinazohusu mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI na maeneo mengine kama vile uimarishaji wa mifumo ya kutolea huduma za afya.

