Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa(NBS), Bi.Ruth Minja, akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu hali ya Mfumuko wa Bei kwa Mwaka ulioishia Februari 2020, Mkutano ulifanyika Ofisi za Takwimu Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa(NBS), Bi.Ruth Minja, akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani), kuhusu hali ya Mfumuko wa Bei kwa Mwaka ulioishia Februari 2020, Mkutano ulifanyika Ofisi za Takwimu Jijini Dar es Salaam.
Picha na Idara ya Habari-MAELEZO.
***************************
Na.Mwandishi Wetu-MAELEZO.
Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa mfumuko wa bei wa taifa umezidi kuimarika kwa mwaka ulioishia mwezi Februari, 2020 baada ya kubaki palepale kwenye asilimia 3.7 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioshia Januari 2020.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Bi.Ruth Minja alisema kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioushia mwezi Februari, 2020 imebaki kuwa sawa na kasi ya iliyokuwepo mwezi Januari, 2020.
“Hali hii ya mfumuko wa bei kubaki kuwa sawa kama ilivyokuwa mwezi Januari imechangiwa na kuongezeka na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula
na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia Februari 2020”, alisema Bi. Ruth Minja.
Aidha ameongeza kuwa kuna baadhi ya bidhaa za vyakula kama nyama ambayo iliongezeka kwa asilimia 1.6, samaki 6.1, mafuta ya kupikia 2.8, maharage 9.3 na viazi vitamu 4.2. Ongezeko la bei ambalo limekuwepo kwa Februari 2020 ni sawa na ongezeko hilo Februari 2019.
Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilipungua bei kwa mwezi Februari, 2020 zikilinganishwa na bei za mwezi Februari, 2019 kama vile jiko la gesi ya kupikia lilipungua kwa asilimia 1.6, viatu vya watoto asilimia 1.0, mafuta ya nywele za wanawake asilimia 2.5 na gharama za huduma za starehe asilimia 1.0.
Minja alibainisha kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioisha mwezi Februari, 2020 umeongezeka hadi asilimia 5.9 kutoka
asilimia 5.7 kwa mwaka ulioishia Januari 2020.
Aliitaja Tanzania katika Nchi za Afrika Mashariki kuwa imeendelea kuwa vizuri kwenye mfumuko wa bei kwa asilimia 3.7 ikilinganishwa na Kenya asilimia 6.37
kutoka asilimia 5.78, wakati Uganda mfumuko wa bei umebakia pale pale 3.4 kwa mwaka ulioishia Januari 2020.