Na Neema Mtuka Sumbawanga 

Rukwa:Kamati ya Maafa ya Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imefika katika Kata ya Senga manispaa ya Sumbawanga kwa ajili ya kufanya tathmini ya madhara yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na mawe.

Mvua hiyo iliyonyesha jioni ya Januari 16, 2026 imesababisha nyumba moja kuezuliwa paa pamoja na watoto wawili kujeruhiwa.

 Kamati hiyo imewapa pole wananchi waliopatwa na tukio hilo na kuwataka kuendelea kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua kubwa.

Mmoja wa mashuhuda katika tukio hilo Magalu Ngasa amesema alishuhudia wakati nyumba hiyo inaezuliwa.

Ngasa amesema ni muhimu kuchukua tahadhari pindi mvua zinaponyesha ili kuepuka madhara kama hayo.

” Kuchukua tahadhari ni muhimu kwa kuwa niliwaona watoto hao wakiwa nje wakati mvua inanyesha ,tuepuke kukaa sehemu hatarishi kama kwenye miti wakati mvua zinaponyesha.”amesema Ngasa.

Amesema watoto hao wakiwa wanachunga ng’ombe wakati mvua ikiwa inanyesha walisimama kwenye ukuta ambao ulidondoka na mtoto mmoja kuvunjika kiuno na mwingine mguu.

Aidha, kamati inasisitiza wananchi kuzingatia ujenzi bora, kupanda miti kwa ajili ya kupunguza kasi ya upepo, pamoja na kulinda mazingira ili kuepuka mmomonyoko wa udongo.

Kwa mujibu wa tathmini kamili, hakuna vifo vilivyoripotiwa kutokana na tukio hilo, isipokuwa watoto wawili waliojeruhiwa ambao wanaendelea kupatiwa matibabu.

Kaimu mkurugenzi ya Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Mussa Musoma ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya maafa amesema wananchi wawe watulivu katika kipindi hiki ambacho serikali inaendelea kushughulikia madhara hayo.

“Serikali ipo kazini kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.” amesema Musoma