Na. Fullshangwe Media
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amehutubia taifa akiwa Ikulu Ndogo Tunguu Zanzibar wakati wa Mkesha wa kuuaga Mwaka 2025 na kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2026, tarehe 31 Desemba, 2025.
Katika hotuba yake, Rais Dkt. Samia amesema kuwa akiba ya fedha za kigeni imeimarika na sasa inatosheleza uagizaji wa bidhaa zaidi ya miezi mitano. Aidha, amebainisha kuwa serikali imejizatiti kuongeza umakini katika usimamizi wa fedha za umma na kuongeza mapato ili kuendeleza ukuaji wa uchumi.
Aidha, Rais amebainisha kuwa Pato la Taifa limeongezeka kwa asilimia 0.6, huku mfumuko wa bei ukidhibitiwa, na Deni la Taifa likibaki kuwa himilivu. Hali hii inaashiria maendeleo chanya katika sekta za kiuchumi nchini.
Aidha, Rais amebainisha kuwa katika kuukaribisha mwaka mpya wa 2026, taifa limeondokewa na wapendwa wake na hivyo kuwaomba wananchi waendelee kuwaombea. Ameongeza kuwa umoja wa kitaifa unabaki kuwa ajenda kuu ya mwaka huu mpya.
Rais amebainisha kuwa serikali inaweka mazingira rafiki ya kisera na kisheria ili kuongeza fursa za uwekezaji huku ikilinda rasilimali za nchi. Aidha, ameeleza kuwa serikali inaendelea kukamilisha miradi ya maji inayolenga kumaliza kabisa tatizo la maji jijini Dar es Salaam.
Aidha, Rais amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha na kudumisha ushirikiano wa kimataifa na kikanda, ikitumia diplomasia ya uchumi kuvutia uwekezaji, kukuza biashara na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Aidha, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa Watanzania hawapaswi kuruhusu tofauti za kiitikadi au kimtazamo kuwagawa na kuwapotezea malengo ya taifa, na amebainisha kuwa umoja wa kitaifa unabaki kuwa ajenda kuu ya Taifa mwaka 2026.
