Na. Fullshangwe Media

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa wananchi wa Tanzania wanapaswa kusherehekea sikukuu za mwaka 2026 kwa amani, kudumisha upendo na kuendeleza amani nchini.

Akilihutubia Taifa kwenye Mkesha wa kuuaga Mwaka 2025 na kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2026 uliofanyika Ikulu ndogo Tunguu Zanzibar tarehe 31 Disemba, 2025, amesema kuwa mwaka 2026 Tanzania itaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 kwa kuzingatia malengo ya kipindi kifupi cha miaka mitatu.

Aidha amebainisha kuwa ndani ya siku 100 za kwanza Chama Cha Mapinduzi kiliahidi wakati wa kampeni kufanya mambo kadhaa katika siku hizo, amebainisha kuwa Serikali itatoa taarifa ya utekelezaji wake mwezi Februari 2026.

Amesema kuwa kutokana na uhaba wa mvua uliosababisha changamoto ya maji, amewapa pole wakazi wa Dar es Salaam na maeneo yote yaliyokumbwa na changamoto hiyo. Aidha amebainisha kuwa Serikali ilielekeza ukarabati wa vyanzo vya maji vilivyokuwa karibu ili kuondoa changamoto hiyo kwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani.

Rais Samia amesema kuwa mwaka 2025 Taifa lilipitia changamoto mbalimbali, Aidha amevishukuru vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi kwa kuendelea kudumisha amani nchini.

Aidha amebainisha kuwa Serikali imejipanga kuunda Tume ya Maridhiano mwaka 2026, akisisitiza kuwa Taifa lisikubali kugawanywa kwa misingi ya itikadi au udini, huku akisisitiza kuwa amani na mshikamano ni tunu ya Mtanzania.

Amesema kuwa mwaka 2026 Serikali itaendelea kuimarisha uhusiano wa kikanda na kimataifa.