*Msaada wa magodoro 100 walenga kuboresha ustawi wa wafungwa Kilindoni na Kilombero; DC apongeza, asisitiza usimamizi

𝐌𝐚𝐟𝐢𝐚. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umekabidhi magodoro 100 yenye thamani ya Shilingi milioni 5.5 kwa Jeshi la Magereza wilayani Mafia, hatua inayolenga kuboresha ustawi wa wafungwa katika magereza ya Kilindoni na Kilombero.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, aliipongeza TFS kwa mchango huo akisisitiza kuwa magodoro hayo yatatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa na kuahidi usimamizi madhubuti wa mali hiyo ya umma.

Awali, akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Profesa Dos Santos Silayo, Kamanda wa Kanda ya Mashariki wa TFS, Mathew Ntilicha, alisema lengo la hatua hiyo ni kuchangia maendeleo ya jamii wilayani Mafia, akibainisha kuwa taasisi hiyo inaamini katika kurejesha kwa jamii.

Aliongeza kuwa shughuli za kijamii zina uhusiano wa moja kwa moja na juhudi za uhifadhi wa misitu na mazingira, na kusisitiza kuwa TFS itaendelea kushirikiana na jamii pamoja na taasisi za serikali katika miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza wilayani Mafia, Gastory Suline, aliishukuru TFS kwa msaada huo na kueleza kuwa magodoro yatatumika ipasavyo kwa manufaa ya wafungwa, akipongeza mchango wa wakala huo katika kuimarisha ustawi wa taasisi za magereza.