Kesi za waliokuwa wagombea 14 wa Ubunge kupitia Chama cha ACT-Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 zinatarajiwa kuanza kutajwa kwa mara ya kwanza leo, Disemba 15, 2025, katika Mahakama Kuu ya Zanzibar Kanda ya Pemba.
Wagombea hao wamefungua kesi dhidi ya Wasimamizi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiwalalamikia kwa madai ya kukiuka taratibu na sheria za uchaguzi, pamoja na matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola wakati wa mchakato wa uchaguzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walalamikaji hao wamesema wameamua kwenda mahakamani kama sehemu ya mapambano ya kudai haki yao ya kidemokrasia.
“Tupo katika kupigania haki yetu, na tunaamini Mahakama zitatenda haki,” alisema mmoja wa waliowasilisha kesi hizo.
Kesi hizo zinafuatiliwa kwa karibu na wadau mbalimbali wa siasa na haki, hasa visiwani Pemba, zikitarajiwa kuwa na athari kubwa katika mjadala wa haki na uhalali wa uchaguzi wa mwaka 2025.

