Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Angola hapa nchini Mhe. Domingos De Almeida Da Silva Coelho, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 11 Desemba 2025.

………….. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amepokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Mabalozi wapya watano walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao, katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma.

Mabalozi waliowasilisha hati za utambulisho ni:

1. Mheshimiwa Domingos de Almeida da Silva Coelho, Balozi wa Jamhuri ya Angola;

2. Mheshimiwa Marjo Johanna Jacoba Crompvoets, Balozi wa Ufalme wa Uholanzi;

3. Mheshimiwa Mohammad Javad Hemmatpanah, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran;

4. Mheshimiwa Ivan Lančarič, Balozi wa Jamhuri ya Slovakia; na

5. Mheshimiwa Gabriel Pandureni Sinimbo, Balozi wa Namibia nchini Tanzania.

Rais Samia aliwakaribisha Mabalozi hao na kusisitiza dhamira ya Tanzania kuendeleza uhusiano wa kirafiki na ushirikiano unaojengwa juu ya kuheshimiana, malengo ya pamoja ya maendeleo na historia ya mahusiano kati ya Tanzania na nchi wanazotoka.

Aidha, alibainisha kuwa Tanzania ina nia ya dhati ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji, hususan katika maeneo yenye fursa kama vile kilimo, uongezaji thamani mazao, nishati pamoja na maji.

Rais Samia pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika sekta za afya, elimu, uchumi wa buluu, utalii, teknolojia.

Katika sekta ya elimu, alieleza dhamira ya Serikali ya kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana kupitia ushirikiano na nchi zenye utaalamu wa kiteknolojia ili kuwapatia vijana ujuzi utakaowezesha kuajiriwa au kujiajiri.

Aidha, Rais Samia alizipongeza nchi hizo kwa mchango wao katika safari ya maendeleo ya Tanzania, na kuhimiza ushirikiano wa kina zaidi unaoendana na Dira 2050 na Sera ya Mambo ya Nje inayotilia mkazo diplomasia ya uchumi, ushirikiano wa kimkakati na ushiriki hai katika majukwaa ya kikanda na kimataifa.

Katika hatua nyingine, Rais Samia aliwahakikishia Mabalozi hao hali ya amani, utulivu na usalama nchini, akisisitiza kuwa Tanzania inabaki kuwa mahali salama kwa wananchi wake, wawekezaji na wafanyabiashara.

Alimalizia kwa kuwahakikishia Mabalozi hao ushirikiano kamili kutoka kwa Serikali ya Tanzania wanapoanza majukumu yao, sambamba na matumaini kwamba uwepo wao utazaa fursa mpya za ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili.

Taarifa Zaidi:

Ushirikiano na Jamhuri ya Angola:

Ushirikiano unahusisha sekta za biashara, nishati, madini, uchumi wa buluu, mifugo na utalii.

Ushirikiano na Uholanzi:

Ushirikiano unahusisha sekta za kilimo, afya, elimu, uvuvi, maji na uwekezaji.

Ushirikiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran:

Ushirikiano unajumuisha sekta za biashara, nishati, teknolojia, kilimo, afya na elimu.

Ushirikiano na Jamhuri ya Slovakia:

Ushirikiano unaakisi maeneo ya nishati jadidifu, ubunifu wa kidijitali, uzalishaji viwandani, usalama wa mtandao, elimu na utalii. Aidha, Slovakia imefungua hivi karibuni ubalozi wake nchini Tanzania, hatua inayochochea ushirikiano wa muda mrefu wa kiuchumi na maendeleo.

Ushirikiano na Jamhuri ya Namibia:

Ushirikiano unahusisha biashara, uchumi wa buluu, nishati, madini, mifugo na utalii. Halikadhalika, ugunduzi wa mafuta na gesi nchini Namibia ni fursa ya kujenga uwezo wa pamoja na ushirikiano katika mnyororo wa thamani wa nishati katika siku zijazo.

Shaaban Kissu

Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Balozi Mteule wa Uholanzi hapa nchini Mhe. Marjo Johanna Jacoba Crompvoets, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 11 Desemba 2025

Balozi Mteule wa Jamhuri ya Iran hapa nchini Mohammad Javad Hemmatpanah akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili Ikulu Chamwino mkoani Dodoma kwa ajili ya kuwasilisha Hati zake za Utambulisho tarehe 11 Desemba 2025

Balozi Mteule wa Jamhuri ya Slovakia hapa nchini Mhe. Ivan Lancaric akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili Ikulu Chamwino mkoani Dodoma kwa ajili ya kuwasilisha Hati zake za Utambulisho tarehe 11 Desemba 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Namibia hapa nchini Gabriel Pandureni Sinimbo, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 11 Desemba 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Angola hapa nchini Mhe. Domingos De Almeida Da Silva Coelho, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 11 Desemba 2025.