…………………………………………………………………………………………………………
Waandishi wa habari watatu nchini Tanzania, ambao pia ni wamiliki wa runinga mtandaoni, leo Machi 04, 2020 wamefikishwa kwenye mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, ambapo kila mmoja anakabiliwa na shitaka moja la kuweka maudhui mtandaoni bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Waandishi hao, ambao tangu kukamatwa kwao walinyimwa haki ya dhamana ni; Prosper Daudi Mfugale, ambaye ni mwandishi wa kituo cha runinga cha ITV na mmiliki binafsi wa runinga ya mtandaoni ya Njombe TV.
Mwandishi mwingine ni Ibrahim Godfrey Mlele, ambaye mwandishi wa kituo cha runinga cha TV E na mmiliki wa runinga ya mtandaoni ya Mlele TV, pamoja na mwandishi Dickson Kanyika, ambaye anafanya kazi na kituo cha runinga cha Star TV na kumiliki runinga yake mtandaoni inayojulikana kama Habari Digital TV.
Mbali na waandishi hao watatu, mtu mwingine aliyekamatwa pamoja na waandishi hao na kufikishwa mahakamani hapo leo ni Benedict Kisawa, ambaye ni mmiliki wa runinga mtandaoni inayofahamika kama Njombe Yetu TV.
Wakiwa mbele ya mahakama hiyo leo, waandishi hao watatu pamoja na mmiliki huyo mmoja wa runinga mtandaoni kila mmoja amesomewa shitaka lake na kupangiwa hakimu wake atakayesikiliza kesi yake.
Hata hivyo, waandishi wote watatu pamoja na mmiliki huyo wa runinga wameshtakiwa kwa kosa linalofanana, ambapo wamedaiwa kuchapisha habari mtandaoni bila ya kuwa na leseni kutoka TCRA.
Kwa mujibu wa kifungu namba 130 (1) cha Sheria ya Mawasiliano ya Mtandaoni na Posta Sura ya 306 (Toleo la Mwaka 2017) pamoja na kanuni ya 14 (1) na 18 ya Kanuni za Mawasiliano ya Mtandaoni na Posta (Maudhui ya Mtandaoni) za mwaka 2018 ni kosa kutoa taarifa mtandaoni bila kuwa na leseni kutoka TCRA.
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), ambao hutetea wanaharakati wa haki za binadamu nchini humo wakiwemo wanahabari umelaani vikali kitendo cha wanahabari hao kukamatwa, ambapo umedai kuwa kimsingi kitendo hicho kinalenga kuendelea kuminya haki ya uhuru wa watu kujieleza kwa kutumia njia yoyote ikiwemo mitandao.
Mwaka 2018 Mtandao huo wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini Tanzania ukishirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT) pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) ulifungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania ukipinga kanuni za Maudhui ya Mtandaoni kwa madai kuwa kanuni hizo, kwa kiwango kikubwa zinaminya uhuru wa watu kujieleza, jambo ambalo ni kinyume na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.