Kamishna wa Operesheni na mafunzo Jeshi la Polisi Liberatus Sabas pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki nchini Profesa Lazaro Busagala wakionyesha hati za Makubaliano ya kutoa Ulinzi na Tume ya Nguvu za Atomik Tanzania jana jijini Arusha
Kamishna wa Operesheni na mafunzo Jeshi la Polisi Liberatus Sabas akizungumza katika hafla hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki nchini Profesa Lazaro Busagala akizungumza katika hafla hiyo.
…………………………………………………………………………………
Jeshi la Polisi nchini limeingia Makubaliano ya kutoa Ulinzi na Tume ya Nguvu za Atomik Tanzania, kutokana na eneo hilo kuwa ni muhimu kwa nchi,pamoja na usalama wa nchi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa eneo hilo halitumiwi na wahalifu.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo jijini Arusha leo Kamishna wa Operesheni Liberatus Sabas alisema kuwa eneo hilo ni muhimu sana kwa usalama wa nchi hivyo, linahitaji kuwa salama na ulinzi mathubutu ili kuzuia wahalifu kutotumia eneo hilo.
Sabas alisema kuwa ikiwa ulinzi hautaimarishwa katika eneo hilo linaweza kusababisha vitu vinavyopatika katika eneo hilo la Tume ya Nguvu za Atomiki kutumiwa vibaya na wahalifu na kupelekea kuleta athari kwa nchi.
Aidha alisema kuwa ulinzi wa eneo hilo ni pamoja na kuhakikisha eneo linakuwa salama ikiwa ni pamoja na wafanyakazi na nchi kwa ujumla.
“Mkataba huo tuliotiliana saini sio mpya kabisa ni utaratibu wa kila mwaka kati ya Jeshi la Polisi na Tume ya Nguvu za Atomiki, ambapo lengo lake ni kuboresha Uhusiano baina ya taasisi hizo kwa Maslahi Mapana ya nchi.””alisema Sabas.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki nchini Profesa Lazaro Busagala alisema kutokana na mkataba waliousaini leo wana matarajio makubwa hasa ya kupanua wigo wa mahusiano baina ya tume ya nguvu za atomiki na jeshi la Polisi kwa ujumla.
“Kuna maeneo ambayo yanahitaji ulinzi zaidi na maeneo ambayo yanahitaji usalama zaidi hivyo leo tumepanua wigo zaidi na matarajio yetu sasa hivi ni kuhakikisha kuwa Tanzanian inakuwa salama”alisema Profesa Busagala.
Profesa Busagala alisema kuwa makubaliano hayo yameendelea kupanua wigo hivyo taifa litakuwa salama haswa kwa upande wa mionzi ama nyuklia kuptia ushirikiano na jeshi la hilo la Polisi.