Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu akiwasilisha taarifa ya hali ya lishe katika mkoa mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga aliyemuwakilisha Mkuu wa mkoa pamoja na wadau wa maendeleo katika mkoa wa Rukwa
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura pamoja na Mgeni Rasmi wa Warsha hiyo Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule wakiwa wameshika na kuviangalia miongoni mwa vifaa vinavyotumika kupimia utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano
Baadhi ya wadau wa maendeleo waliohudhuria kwenye warsha ya kujadili namna ya kutokomeza udumavu katika mkoa wa Rukwa
Baadhi ya wadau wa maendeleo waliohudhuria kwenye warsha ya kujadili namna ya kutokomeza udumavu katika mkoa wa Rukwa
Mkurugenzi wa Taasisi ya Hodari International Ltd Ted Rabenold akichangia mawazo yake katika warsha ya wadau wa maendeleo kuhusiana na namna ya kutokomeza udumavu katika mkoa wa Rukwa.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule akiongea na wadau waliohudhuria kwenye warsha ya lishe (hawapo pichani) katika mkoa wa Rukwa
……………………………………………………………………………………………
Wadau mbalimbali wa maendeleo katika Mkoa wa Rukwa wamekutanishwa katika warsha ya wadau wa lishe ili kuhakikisha wanajadili na kushirikiana juu ya utekelezaji wa afua za lishe ndani ya mkoa huo na hatimae kutokomeza utapiamlo unaopelekea zaidi ya watoto 90,000 walio na umri wa chini ya miaka mitano kuwa na udumavu
Katika kikao hicho kilichoongozwa na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule aliyemuwakilisha mkuu wa mkoa wa Rukwa alisema kuwa mbali na mpango mkakati jumuishi wa miaka mitano (2016-2021) wa kitaifa wa kupambana na tatizo la lishe kuzitaka halmashauri kuchangia shilingi 1,000 kwa kila mtoto pia kama wadau wa maendeleo jitihada zao zinahitajika katika kupunguza udumavu kwa lengo la kuboresha lishe kwa wananchi wa mkoa huo.
Na kuwakumbusha kuwa mpango huo wa kitaifa na wa mkoa unajumuisha wadau wa sekta mbalimbali za serikali na za kiraia kwa kuwa na ufahamu kuwa suala la lishe ni suala mtambuka na hivyo mafanikio ya kudhibiti udumavu mkoani humo yanategemea pia nguvu ya wadau na hilo ndio lengo la kuwaita washiriki hao ili kuonesha kuwa suala hilo linamgusa kila mmoja kwa nafasi yake.
“Wote tutambue kuwa maendeleo ya Taifa letu, pamoja na mambo mengine, yanahitaji watu wenye afya njema na hali bora ya lishe, ili kufanikiwa hilo tunatakiwa kuwa na uelewa wa kina wa sababu za lishe duni katika kila eneo la mkoa wetuna kubuni mikakati ya kukabiliana na aina zote za utapiamlo katika jamii zetu, jambo hili litafanikiwa endapo elimu sahihi ya lishe itatolewa na kuimarisha ushiriki wa kila sekta, kila mdau na kila mtu katika nafasi yake,” Alisisitiza
Pia alisisitiza kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 lakini lishe duni imeendelea kuathiri maendeleo yetu ya kiafya, kielimu na kiuchumi na kusababisha kasi ya uchumi wetu kuku ana kupungua kwa umasikini nchini kuwa si ya kuridhisha na kuongeza kuwa lishe duni hupunguza nguvu kazi ya taifa na kuongeza gharama ya matibabu kutokana na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukizi.
Wakati akiwasilisha changamoto mbalimbali za mkoa katika utekelezaji wa afua za lishe Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu alisema kuwa jamii ina uelewa mdogo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu lishe hasa katika utayarishaji wa chakula na matumizi ya lishe anuwai (diversified dietary)
“Miongongoni mwa changamoto za mkoa huu ni pamoja na ushirikishwaji mdogo wa wadau ndani ya mkoa, hususan sekta binafsi, katika kutekeleza afua za lishe lakini pia mkoa kutokuwa na mifumo Madhubuti ya kufuatilia na kusimamia mchango wa sekta binafsi katika eneo la lishe pamoja na halmashauri kutotoa fedha kwa wakati ili kuwahudumia Watoto lakini la Zaidi tunahitaji mdau anayeweza kufanya “fortification” ndani ya mkoa, tuna upungufu wa vifaa vya kufanyia tathmini ya hali ya lishe kwa Watoto,” Alisema
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mradi wa Lishe Endelevu Dkt. Joyceline Kaganda alisema kuwa wengi waliohudhuria kwenye warsha hiyo wanaweza kuwa na hali nzuri kimaisha lakini kwa namna moja ama nyingine jamii inayowazunguka wanaishi katika lishe duni inayopelekea utapiamlo mkali.
“Unaweza ukawa vizuri lakini wanaokuzunguka katika eneo unaloishi wanahali mbaya san ana pengine unahudhuria hata mazishi ya Watoto ambao wanakufa kwa utapiamlo mkali lakini ungeweza kufanya hii kitu ukaokoa Maisha ya watoto hao, kwahiyo mimi niseme asante kwa mwanzo huu tuliouanza kuna wadau wengi tuliwaita, wadau wa elimu hawajaongea, wadau wa mabenki wengine hawajafika, hii shughuli ya kutatua tatizo la utapiamlo ni mtambuka, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kufanya kitu,” alisisitiza.
Miongoni mwa wadau waliohudhuria katika warsha hiyo Mkurugenzi wa Taasisi ya Hodari International Ltd Ted Rabenold alisema kuwa yupo tayari kushirikiana na jamii ya wanarukwa kuhakikisha anawapatia miti ya matunda ya kutosha pamoja na kutoa mafunzo mmbalimbali juu ya namna ya kuwa na kilimo chenye tija katika mashamba na kuwataka wadau hao kushirikiana kwa dhati ili kutokomeza udumavu katika mkoa.