………………………………………………………………………………………….
Yanga imeutumia vyema uwanja wake wa nyumbani kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbao FC toka Mwanza mechi iliyomalizika katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.
Mshambuliaji kutoka Congo David Molinga aliwanyanyua mashabiki wa Yanga dakika ya 28 akifunga bao kwa mkwaju wa Penalti mara baada ya beki wa Mbao FC kumchezea rafu Fei Toto.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Yanga kwenda mapumziko wakiwa na uongozi wa bao moja huku ikitumia kikosi cha pili na kuwaacha nyota wake nje kujiandaa na mechi ya watani wa jadi Simba siku ya Jumapili Machi 8.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko huku Yanga wakinufaika na mabadiliko hayo kwani waliweza kupata bao la pili.
Baada ya kukosa kosa kufunga kipindi cha pili Kiungo Mshambuliaji Patrick Sibamona aliifungia Yanga bao dakika ya 81 akimalizia pasi ya Mapinduzi Balama aliyeingia kutoka benchi.
Kwa ushindi huo Yanga wamefikisha Pointi 47 na kukwea hadi nafasi ya tatu na kuishusha Namungo FC huku Azama wakiwa nafasi ya pili kwa Pointi 48 na vinara wa Ligi Simba bado wanaongoza Msimamo kwa Pointi 65.
Mechi za Ligi Kuu Vodacom Tanzania bara zinatarajia kuendelea kesho kwenye viwanja mbalimbali huku macho ya wengi yatakuwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam Azam Fc watawaalika vinara Simba majira ya saa moja jioni.