Mratibu mkuu taasisi ya TONISA (katikati) ndugu. Salum Kasim Takadiri akiwa na msaidizi wake (kulia) ndugu Abubakar Khamis pamoja na mwana kamati wa tamasha la usiku wa mwana Dodoma (kushoto).
…………………………………………………………………………………………….
Na.Boniphace Richard,Dodoma
Taasisi inayojihusisha na masuala ya kijamii, jijini Dodoma (TONISA) imeandaa ufunguzi wa tamasha la usiku wa mwana Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, mratibu msaidizi wa taasisi hiyo ndugu. Abubakar Khamis amesema kuelekea uzinduzi wa tamasha hilo utakaofanyika tarehe 22 mwezi huu utaangazia masuala mazima ya mji wa Dodoma zikiwemo fursa pamoja na maendeleo mbalimbali ya uwekezaji ndani ya jiji la Dodoma.
“Mwana Dodoma Special Night Event”
Ufunguzi huo utaambatana na utoaji wa tuzo, ikiwemo tuzo ya heshima kwa watu au viongozi waliofanikisha kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya Nchi ambapo tuzo moja wapo itatolewa kwaajili ya ayati baba wa taifa mwl. Julius K. Nyerere kwani ndiye mwasisi wa kwanza katika kuisemea Dodoma kuwa makao makuu ya Nchi.
Tuzo nyingine itatolewa kwa Rais wa awamu ya tano dkt. John Pombe Magufuli, kwa kufanikisha jitihada za kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya Nchi hadi sasa pamoja na tuzo moja kwa bunge la Tanzania sambamba na spika wa bunge tukufu la Tanzania Mhe. Job Ndugai kupewa tuzo ya heshima kwa kufanikisha mjadala wa Dodoma kuwa mako makuu ya Nchi.
Pia tuzo nyingine itatolewa kwa mkuu wa mkoa wa Dodoma dkt. Binilithi Mahenge, ndugu Godwin Kunambi mkurugenzi wa jiji la Dodoma pamoja na vikundi mbalimbali vya wasanii kwa kazi nzuri wanayofanya katika kutunga nyimbo zenye kusifu jiji la Dodoma.
Aidha mratibu msaidizi wa TONISA, ameongeza kuwa lengo la tamasha hilo ni kutoa fursa kwa wawekezaji mbalimbali Nchini kuwekeza katika fursa mbalimbali za kimaendeleo kwa kushirikiana na wajasiliamali ndani ya jiji la Dodoma.
Kwa upande wake mratibu mkuu wa taasisi hiyo, ndugu. Salum Kasim Takadiri amesema kuwa tamasha hilo litahusisha wakuu wa mikoa jirani kwani tamasha hilo ni kwaajili ya maslahi ya taifa kwa ujumla pamoja na uwepo wa wawekezaji wakubwa kama vile Modewij na wengine.
Uzinduzi wa tamasha hilo utafanyika tarehe 22, mwezi huu katika ukumbi wa MORENA walengwa wakuu wakiwa wajasiliamali katika kufungua fursa mbalimbali katika Nyanja ya maendeleo ya jiji la Dodoma.