……………………………………………………………………………………………………
NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
NAIBU Katibu Mkuu Taifa,CCM Rodrick Mpogolo ,amewapa salamu wapinzani wa ndani ya Chama ama wa Vyama vingine vya upinzani wamuache Rais dk.John Magufuli afanye kazi na amewashangaa wanaojaribu kupimana nae ubavu ,wajue wamechemsha.
Pamoja na hilo ,ameeleza mabalozi wa chama ndio mpango mzima na mashina ndio nguvu ya chama hivyo kuna kila sababu ya kuwaheshimu na kuwathamini mabalozi hao katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa Jimbo la Kibaha Mjini, mkutano ambao mbunge Silvestry Koka alipata wasaa wa kueleza utekelezaji wa ilani ,Mpogolo alisema Rais ni mtu wa vitendo, anatekeleza na zipo nchi zinatamani utendaji kazi wake hivyo tuendelee kumuamini .
Alieleza ,mwenyekiti wa CCM Taifa anatekeleza mambo makubwa ya kiuchumi na kimaendeleo kwa maslahi ya watanzania,sasa akitokea ambae haoni yanayofanywa atakuwa ana shida.
“Wapo baadhi ya watu wakipata madaraka wanasahau kuheshimu wenzao,na wengine wakiomba kura wakipata wanajisahau wale waliowapa kura”CCM ni kuheshimiana kiongozi anapaswa kumheshimu mwanachama na mwanachama amuheshimu kiongozi”nina wakumbusha alisema Mpogolo.
Katika hatua nyingine, alisema chama kinaendelea kuwajibisha wale wanaokiuka kanuni na taratibu na bado kipo imara na hakijatikisika.
Hata hivyo,naibu katibu mkuu huyo alisema nguvu ya mamba ipo kwenye maji na nguvu ya CCM ipo kwenye mashina hivyo hatuwezi kushinda vita ya uchaguzi kama tutawatenga mabalozi.
“Viongozi wote kuanzia mkoa,wilaya ,kata wote tupo chini ya mabalozi, hawa mabalozi ndio tunapaswa kuwaheshimu ,wao ndio nguvu ya chama na ndio ushindi wetu”:alisisitiza Mpogolo.
Mpogolo alimpongeza Koka kwa utekelezaji wa ilani ,na mwenye macho aambiwi tazama ,mbunge ni utekelezaji sio kutoa vijisenti kwa mtu mmoja mmoja.
“Sijaja kumpigia debe Koka ila amefanya kazi ,nimeshuhudia ambulance aliyoitoa na pikipiki na mengine mengi anayoyafanya kwa maslahi ya jamii”alisema Mpogolo.
Awali mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini,Silvestry Koka alikabidhi pikipiki 14 katika kata ambapo kila moja imegharamia milioni 2.5 na gari la wagonjwa ambalo litasaidia katika dharura hospital ya Mkoani.
Koka alielezea kwamba, licha ya hayo asilimia 58 ya mfuko wa jimbo imeelekezwa katika sekta ya elimu ili kutatua changamoto za kielimu.
Wakati huo huo , alieleza kuwa,serikali imefanya kazi kubwa kwenye sekta ya afya kwa kujenga hospital ya wilaya na kuimarisha utawala bora ,nishati,afya,usalama na kwasasa asilimia 84 ya wakazi Jimbo la Kibaha Mjini ,wanapata maji .
Nae mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini,Maulid Bundala alisema, wamejipanga kushinda uchaguzi wa kata ,jimbo na Rais na kuwataka wana Kibaha wafikie hatua ya kuwa na fadhila kwa kushukuru namna walivyoshirikiana kutatua baadhi ya chanagamoto na mbunge kwa kipindi cha uongozi wake.
“Na leo amekabidhi pikipiki 14 zitakazosambazwa katika kata zote na ametoa gari la wagonjwa hospital ya Mkoani ,Tuwe na fadhila kwa kidogo tunachopatiwa,Hatusemi kisa mseme tunamfagilia ila anapofanya mtu na kutekeleza lazima sifa apewe”alisisitiza Bundala.
Mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama alisema ,wanajivunia kuwa na umoja na chama na serikali na kutekeleza ilani ya chama kwa asilimia 100.
Alieleza Koka anatosha kwani ni mengi amefanya katika Jimbo.