Na John Bukuku – Mnazi Mmoja, Zanzibar
Baada ya kufanya mikutano mikubwa ya kampeni katika mikoa ya Tanzania Bara ikiwemo Dar es Salaam, Pwani na Rukwa, leo Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaendelea na kampeni zake visiwani Zanzibar kupitia mkutano mkubwa wa hadhara unaofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Wananchi wa Zanzibar wamejitokeza kwa wingi katika maandalizi ya kumpokea kiongozi huyo, huku shamrashamra, nyimbo za hamasa na mabango ya kijani na njano yakitawala mitaa mbalimbali ya Mjini Unguja.
Kwa mujibu wa viongozi wa CCM Zanzibar, mkutano wa leo ni miongoni mwa mikutano mikubwa zaidi ya kampeni, ukiwa na lengo la kueleza mafanikio yaliyopatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na kuainisha dira ya maendeleo kwa kipindi kijacho.
Dkt. Samia anatarajiwa kugusia masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya Zanzibar ikiwemo uchumi wa buluu, elimu, afya, utalii, uvuvi, uwezeshaji wa wanawake na vijana, sambamba na kuhimiza uimarishaji wa umoja na mshikamano wa kitaifa.
Aidha, anatarajiwa kuwasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29 kwa amani na utulivu, na baada ya kupiga kura kurudi majumbani kwa amani wakisubiri matokeo, kama ishara ya kudumisha utulivu na heshima ya taifa.
