……………………………………………………………………………………………………..
NA MWAMVUA MWINYI, PWANI
MKUU wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama amewaasa wazazi na walezi , wilayani hapo kuwekeza katika elimu kwa watoto wao ili kuondokana na ujinga kwa manufaa ya maisha yao ya baadae.
Aidha ameitaka ,jamii kujenga tabia ya kujitolea kuchangia kwenye elimu ili kupunguza changamoto zinazoikabili sekta hiyo badala ya kuiachia serikali na wadau pekee.
Akitoa shukrani zake baada ya kukabidhiwa cheti kwa kupongezwa mchango wake kwenye elimisha Kibaha, cheti ambacho amekabidhiwa na baraza la Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ,alisema wazazi wasiwe sehemu ya kuzima nyota ya elimu kwa vizazi vyao.
“Sijawahi kuishiwa neno lakini leo nakosa neno la kusema, nawashukuru kwa kutambua nilichokifanya, katika kampeni ya ELIMISHA KIBAHA ,ninachowaomba kuzingatia suala la Elimu.
Mshama alisema, hadi sasa kati ya vyumba vya madarasa 65 vilivyokuwa vinahitajika, 20 vimekamilika, ambapo aliwashukuru waliochangia kufanikisha Kampeni ya Elimisha Kibaha.
Akimkabidhi cheti hicho,Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Kibaha Mjini, Edwin Shunda ,alieleza pia mwanachama Rugemarila Rutatina aliyekuwa mjumbe wa Halmashauri kuu ya Wilaya (MNEC) alipatiwa cheti kutokana na mchango alioutoa kwa Jumuiya hiyo.
Shunda alitoa wito ,kwa wazazi kuwa na mwamko katika kuchangia elimu, ili kuunga mkono juhudi za Serikali.
Baraza hilo pia lilijadili utekelezaji wa Ilani pamoja na maandalizi ya uchaguzi mkuu, lengo kufanikisha chama hicho kupata ushindi mwezi Octoba.