NA JOHN BUKUKU- BARIADI SIMIYU

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa hali ya usalama nchini ipo shwari kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, na kuwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura bila hofu.

Akizungumza na wananchi wa mkoa wa Simiyu, Dkt. Samia, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, amewaonya wale wanaotumia picha na taarifa za kutisha kujaribu kuwatia hofu Watanzania, akisisitiza kuwa serikali imejipanga vyema kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu.

“Nataka kuwaambia, ninayezungumza hapa ni Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii. Wasithubutu! Tumejipanga vizuri. Tokeni mkapige kura, rudini nyumbani, hakuna kuogopa,” amesema Dkt. Samia.

Amesema maandalizi yote muhimu yamekamilika, na vyombo vya ulinzi na usalama viko tayari kulinda amani ya nchi kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Aidha, amewashukuru viongozi wa CCM kwa maandalizi mazuri ya kampeni na kueleza kuwa vijana wengi waliokuwa upande wa upinzani sasa wanarejea CCM, jambo linaloashiria umoja na mshikamano wa Watanzania.

Dkt. Samia pia ameeleza kuwa serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta za maji, umeme, elimu, afya pamoja na mradi mkubwa wa reli ya kisasa (SGR) utakaopita mkoani Simiyu, ambao utazalisha ajira na fursa nyingi za biashara.

Amewataka wananchi wa Simiyu na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuiamini na kuipa CCM dhamana ya kuendeleza mafanikio yaliyopatikana chini ya kaulimbiu “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele.”