NA JOHN BUKUKU- MUSOMA
Baada ya kumaliza mikutano ya kampeni jana mjini Musoma, Mkoa wa Mara, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameendelea na muendelezo wa kampeni zake katika miji ya Butiama, Serengeti, na Bariadi mkoani Simiyu.
Katika mikutano hiyo, Dkt. Samia anatarajiwa kuzungumzia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kwenye sekta za maji, barabara, elimu, kilimo, afya na nishati.
Aidha, Dkt. Samia atawahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kupiga kura kwa amani na utulivu, huku akisisitiza umuhimu wa kuichagua CCM ili kuendeleza safari ya maendeleo ambayo tayari imeonesha matokeo chanya katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa ratiba ya kampeni za Chama Cha Mapinduzi, baada ya mikutano hiyo, Dkt. Samia ataendelea na kampeni katika mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kueleza mafanikio ya Serikali na kueleza mwelekeo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025–2030.
Mikutano hiyo inatarajiwa kuvuta maelfu ya wananchi, viongozi wa chama, wabunge, na wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya CCM, ambao watatumia majukwaa hayo kuelezea dhamira ya chama kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu.
