Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wakazi wa Kanda ya Kaskazini kuwa Mkoa wa Arusha utapewa kipaumbele cha kipekee endapo ataaminiwa kuunda serikali baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza leo wilayani Karatu, mkoani Arusha, Dkt. Samia amesema kwa muda mrefu ukanda huo haujapata kutazamwa vizuri na chama tawala, jambo ambalo serikali yake imelenga kulirekebisha kwa vitendo.
“Huko nyuma ukanda wa Kaskazini haukuwa unatizamwa vizuri sana kwa jicho la chama tawala. Lakini sasa, toka juzi nilivyoingia Arusha na ninavyosikia wagombea wanayoyasema pamoja na viongozi wa kimila, naamini ipo haja ya kurudisha heshima ya mkoa huu,” amesema Dkt. Samia.
Amesisitiza kuwa serikali yake itahakikisha heshima ya Arusha inarejea kwa kuimarisha sekta mbalimbali ikiwemo barabara, uwekezaji na utalii, ili mkoa huo uwe mfano wa maendeleo kwa nchi nzima.
