NA MWANDISHI WETU

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema chama chake kimejipanga kuijenga Zanzibar mpya yenye mshikamano, heshima na maendeleo endapo kitapewa ridhaa ya wananchi katika uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza kwenye mikutano ya hadhara, Othman alisema dira ya chama chake inalenga kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wote kwa kuboresha huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, na ajira.

Alisema ACT Wazalendo itahakikisha sekta kuu za uchumi kama vile utalii, bandari na uvuvi zinatoa manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi badala ya kubaki katika ngazi chache za watu wachache. “Mapato ya taifa lazima yatumike kujenga shule bora, hospitali zenye vifaa na kutoa ajira za maana kwa vijana wetu,” alisema.

Aidha, Othman alieleza kuwa ardhi ya Zanzibar italindwa na kutumika kwa manufaa ya wananchi, ambapo mpango wa chama chake utahakikisha matumizi ya ardhi yamepangwa vizuri kwa ajili ya makazi, kilimo na uwekezaji wenye tija.

Kuhusu sekta ya elimu, alisema serikali ya ACT Wazalendo itaandaa mitaala inayolenga kuendana na wakati na mahitaji ya vijana, hasa katika masuala ya teknolojia, bahari, utalii na viwanda vidogo vidogo.

Othman pia aliahidi kuboresha maslahi ya watumishi wa umma kwa kuanzisha mshahara wa chini wa shilingi milioni moja, hatua itakayoongeza ari ya kazi na heshima kwa walimu, wauguzi na kada nyingine muhimu za serikali.

Akizungumzia kilimo cha karafuu, alisema chama chake kitahakikisha zao hilo linapata bei bora na soko la uhakika, ili wakulima waendelee kulithamini na kuliendeleza kama utambulisho wa kiuchumi wa Zanzibar.

Kwa upande wa vijana, ambao ni zaidi ya nusu ya wakazi wa Zanzibar kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022, Othman alisema ACT Wazalendo itawawezesha kupitia mikopo midogo, mafunzo ya ufundi na teknolojia, pamoja na kuondoa changamoto za upendeleo katika ajira.

Alisema vijana wataajiriwa kwa kuzingatia uwezo na taaluma, na wale wanaotaka kujiajiri watapatiwa mikopo na vifaa vya kuanzisha biashara ndogo ndogo.

“Zanzibar iko kwenye hatua muhimu ya kihistoria. Oktoba 29 ni siku ya kufanya maamuzi ya mustakabali wa taifa letu. Ni wakati wa kuandika historia mpya ya Zanzibar ya mshikamano na maendeleo,” alisema Othman.