NA JOHN BUKUKU-PANGANI, TANGA

Mbunge mteule wa kundi la Vijana kutoka Zanzibar, Zainab Abdallah Issa, ametoa shukurani kwa Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutembelea Mkoa wa Tanga na Wilaya ya Pangani katika muendelezo wa kampeni za chama hicho Septemba 29, 2025.

Akihutubia katika mkutano huo, Zainab alisema amepata heshima kubwa kuaminiwa nafasi za uongozi akiwa na umri mdogo, ikiwa ni pamoja na kuwa Mkuu wa Wilaya kwa miaka tisa na kufanya kazi katika Mkoa wa Tanga kwa miaka saba, hususan katika Wilaya ya Muheza. “Pamoja na mgombea wetu wa urais, anapofika Pangani na Muheza, tunasimama pamoja na Tanga,” alisema.

Zainab alisifu jitihada za Dkt. Samia katika ujenzi wa miundombinu mkoani Tanga, akibainisha kuwa barabara ya Tanga–Pangani–Saadani–Bagamoyo na daraja la Mto Pangani tayari yameanza kutekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 245, mradi ambao utakuwa chachu ya kufungua uchumi wa Mkoa wa Tanga.

Aidha, alizungumzia mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa katika wilaya za Pangani, Muheza, Korogwe na Handeni kwa gharama ya shilingi bilioni 175, pamoja na uwekezaji unaoendelea katika Bandari ya Tanga, ambao unaongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi ya mkoa huo.

“Hakuna kijiji, kata, wala wilaya hapa Tanga ambako huwezi kuona alama za maendeleo yaliyotekelezwa na Dkt. Samia. Elimu, afya, umeme, barabara na uwezeshaji wananchi kiuchumi ni ushahidi wa mabadiliko haya,” alisema.

Zainab pia alisisitiza umuhimu wa amani katika maendeleo ya taifa, akiwataka Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Samia. “Hakuna taharuki, hakuna vita, maana maendeleo hupatikana katika nchi yenye amani. Leo, ndani ya miaka minne, tunaona utulivu na uwekezaji unaoendelea,” aliongeza.

Vilevile, alieleza kuwa Dkt. Samia ametoa kipaumbele kikubwa kwa vijana, ambapo idadi kubwa ya nafasi za maamuzi katika Serikali zipo mikononi mwa vijana, ikiwemo Baraza la Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Pia miradi ya viwanda, michezo na uwekezaji imesaidia kuongeza ajira kwa vijana.

Aidha, aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele kumuunga mkono Dkt. Samia ili kuandika historia ya kumchagua mwanamke wa kwanza kuiongoza Tanzania. “Dkt. Samia ni mwanamama shupavu, jasiri na mwenye uthubutu na mapenzi ya dhati kwa taifa lake. Ni wakati wetu sasa, wanawake, tujitokeze kumchagua,” alisema.

Zainab aliongeza kuwa uwekezaji katika sekta ya michezo na utalii umechangia vijana wengi kupata ajira na kukuza vipaji vyao, hatua inayoongeza morali na kukuza uchumi wa taifa. “Tunamshukuru na kumheshimu Rais wetu kwa kuwainua vijana na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa vitendo. Vijana milioni 8.5 wanatarajiwa kupata ajira kupitia ilani ya CCM,” alisema.

Akihitimisha hotuba yake, Zainab aliwaomba Watanzania kumuunga mkono Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 9, akimueleza kama kiongozi pekee mwenye uwezo wa kuendeleza maendeleo ya taifa. “Mgombea wetu wa urais ni dawa ya matatizo ya Watanzania na ndiye anayeweza kuendeleza maendeleo ya nchi,” alisisitiza.