NA JOHN BUKUKU -KIBAHA PWANI

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na kampeni za chama hicho Septemba 28, 2025, mjini Kibaha mkoani Pwani. 

Akizungumza na wakazi na wananchi wa Pwani kwenye uwanja wa Sabasaba, amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo sambamba na reli ya kilomita 100 itakayoziunganisha Bandari ya Bagamoyo na Bandari Kavu ya Kwala pamoja na kongani ya viwanda vya Mkoa wa Pwani.

Aidha, Dkt. Samia amebainisha kuwa Bandari ya Bagamoyo itajengwa sambamba na eneo maalum la kiuchumi litakalovutia wawekezaji wa viwanda vikubwa na vidogo, na kufanya Mkoa wa Pwani kuwa kitovu cha usafirishaji na uwekezaji nchini.

Pia, amesema kuwa miradi hiyo inatekelezwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Reli Tanzania (TRC) pamoja na sekta binafsi, lengo likiwa ni kuongeza fursa za ajira na biashara kwa wananchi.

Aidha, Dkt. Samia amesema kuwa Mkoa wa Pwani umeendelea kushuhudia ukuaji mkubwa wa viwanda, ambapo zaidi ya viwanda 287 vimejengwa, vikiwemo vikubwa na vidogo, na kutoa ajira za moja kwa moja 21,049 na zisizo za moja kwa moja 960,000.

Vilevile, amebainisha kuwa Serikali inatekeleza miradi ya nishati ikiwemo kituo cha umeme Mkuranga na mtandao wa gesi kutoka Kinyerezi hadi Chalinze ili kuhakikisha viwanda na wananchi wanapata umeme wa uhakika kwa maendeleo ya uchumi.

Pia, Dkt. Samia amesema kuwa Serikali imejipanga kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi kwa lengo la kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kujenga nyumba bora na za kisasa kwa bei nafuu, huku Mkoa wa Pwani ukiendelea kuwa mfano katika utekelezaji wa ajenda ya kitaifa ya makazi bora.