Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima akimuonesha sehemu ya maendeleo ya ujenzi wa jengo la hospitali ya Rufaa ya Kwangwa Musoma Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipofanya ziara kukagua ujenzi wa hospitali hiyo jana, Jengo hilo linajengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima akimuonesha sehemu ya maendeleo ya ujenzi wa jengo la hospitali ya Rufaa ya Kwangwa Musoma Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipofanya ziara kukagua ujenzi wa hospitali hiyo jana, Jengo hilo linajengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua sehemu za jengo la hospitali ya Rufaa ya Kwangwa alipofanya ziara kukagua maendeleo ya ujenzi huo jana. Ujenzi wa jengo hilo unafanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).
****************************
Na Munir Shemweta, WANMM MUSOMA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amelitaka Shirika la Nyumba la Tiafa (NHC) kuongeza kasi ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kwangwa iliyopo Musoma mkoa wa Mara ili kukamilika kwa muda uliopangwa.
Hospitali hiyo ya Kwangwa ni ya ghorofa tano yenye shemu tatu (Wing A, B na C) na inarajiwa kuanza kutoa Huduma kwa baadhi ya sehemu kati kati ya mwezi ujao
Dkt Mabula alitoa kauli hiyo jana tarehe 25 Februari mjini Musoma mkoa wa Mara wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo unaofanywa na NHC akiwa katika ziara yake ya siku moja.
Alisema, pamoja na NHC kufanya vizuri katika ujenzi wa jengo la hospitali hiyo ukilinganisha na wakandarasi waliotangulia lakini inapaswa kuongeza kasi ili likamilike katika muda uliopangwa na kuanza kutoa huduma.
Kwa mujibu wa Mabula, Hospitali ya Kwangwa itakayojulikana kwa jina la Mwl Nyerere Memorial Hospital ina historia ndefu kwa kuwa pamoja na kuasisiwa na Rais wa Kwanza Mwalimu Julius Nyerere lakini utekelezaji wake unakamilishwa na serikali ya awamu ya tano.
‘’Ni vyema NHC mkaongeza bidii katika ujenzi wa hospitali hii ili ikamilike kwa haraka kwa kuwa hospitali hii ina historia ndefu na Rais John Pombe Magufuli ameamua ujenzi huu ukamilike kwa kutoa bilioni 15’’ alisema Mabula.
Katika kuhakikisha ujenzi wa hospitali hiyo unakamilika kwa wakati, Naibu Waziri Mabula alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa NHC Dkt Maulid Banyani kusimamia kwa karibu maendeleo ya ujenzi huo sambamba na kupatiwa ratiba ya mpango wa ujenzi na maendeleo yake kila baada ya siku mbili kwa nia ya kufuatilia kwa karibu.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa Dkt Maulid Banyani alimuahakikishia Naibu Waziri Mabula kuwa, ujenzi wa hospitali hiyo sasa utakamilika kwa wakati baada ya changamoto kadhaa ikiwemo ya Mshauri Mwelekezi kupatiwa ufumbuzi.
Kwa Upande wake Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima mbali na kuisifu NHC kwa kufanya mabadiliko makubwa ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa hospitali ya Kwangwa alioueleza kuwa ilikwamwa kwa mara kadhaa.
‘’Toka Shirika la Nyumba la Taifa lianze ujenzi wa hospitali hii mwezi Agosti mwaka jana kuna mabadiliko makubwa ya kasi ya ujenzi na tunataka mjenge kwa wakati na viwango na Machi mwaka huu Huduma ya Mama na Mtoto ianze kutolewa ‘’ alisema Malima.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, hospitali hiyo itatoa huduma kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya ziwa pamoja na nchi jirani sambamba na kutumika kama sehemu ya utalii kutokana na mazingira ya hospitali.
Historia ya Ujenzi wa Hospitali ya Kwangwa iliyopo Musoma mkoa wa Mara inaanzia mwaka 1977 pale Rais wa kwanza wa Mwl Nyerere alipotoa wazo la kujengwa kwake lakini ujenzi huo umekuwa ukikwama kwa nyakati tofauti hadi Rais John Pombe Magufuli alipotoa Shilingi Bilioni 15 kwa lengo la kukamilishwa mradi huo ambapo sasa unatarajiwa kukamilika mwaka huu.