Afisa Mwezeshaji wa mfuko wa Maendeleo ya jamii Nchini(TASAF)wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Avelinius Rwegasira akiongea jana na wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika kijiji cha Tanesco Tunduru mjini wakati wa malipo kwa walengwa hao.
Baadhi ya walengwa ambao ni wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini Tasaf kijiji cha Tanesco wilayani Tunduru wakisubiri malipo.
Picha na Mpiga Picha Wetu,
*******************************
Na Mwandishi Maalum,
Tunduru
JUMLA ya Bilioni 12.4 zimetumika kwa ajili ya malipo kwa walengwa 13,751 wanaonufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kwa kipindi cha miaka 7 tangu kuanza kwake mwaka 2014.
Mratibu wa mfuko wa maendeleo ya jamii wilaya ya Tunduru(Tasaf) Muhidin Shaibu alisema, hayo wakati wa zoezi la malipo ya mwezi March na April 2019 katika kijiji cha Misufuni kata ya Namiungo wilayani humo.
Aidha alisema, katika kipindi hicho Halmashauri imetekeleza miradi ya ajira za muda kwa walengwa kwa kipindi cha miaka mitatu ambapo jumla ya miradi 424 imetekelezwa na walengwa ikiwemo utengenezaji wa mboloea kwa njia ya asili.
Alitaja kazi nyingine zilizo fanyika ni kuaandaa vitalu vya miche,miradi ya uhifadhi mazingira, ufugaji samaki,nyuki, kupanda miti,kuboresha visima vya asili,kuchimba mabwa ya samaki na malambo.
Alisema,mpango wa kunusuru kaya maskini kwa wilaya ya Tunduru ulianza tangu mwaka 2014 na hadi sasa tayari wameshafanya malipo kwa kipindi cha awamu 32 katika vijiji 88 kati ya 157 vinavyotekeleza mpango huo katika awamu ya kwanza.
Alisema, jumla ya kaya 5,111 zimeweza kuanzisha biashara ndogo ndogo kwa lengo la kujiongezea kipato,kaya 7,670 zimejihusisha na kilimo na ufugaji wa mbuzi,kuku,bata na ng’ombe wakati kaya 5,600 zimefanikiwa kuboresha makazi kwa kujenga nyumba za kisasa.
Kwa mujibu wa Muhidin,mbali na mafanikio hayo baadhi ya walengwa wameweza kuanzisha vikundi 913 vya akiba na mikopo, miradi ya uchimbaji mabwawa ya samaki ambayo imewasaidia kupata ujuzi wa kufuga samaki na kuwa wasambazaji wakubwa wa mbegu za samaki na kitoweo cha samaki ndani na nje ya wilaya ya Tunduru.
Alisema, tangu mradi ulipoanza mwaka 2014 kumekuwa na mabadiliko makubwa yaliyofikiwa kwenye kaya hizo ikiwemo kuongezeka kwa wanafunzi shuleni,kuhudhuria kliniki na kaya kuwa na uhakika wa kupata milo mitatu kwa siku tofauti na siku za nyuma hivyo kupungua kwa kiwango kikubwa tatizo la udumavu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Baadhi ya wanufaika wa mpango huo wameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za ruzuku ambazo zitawasaidia kuwajengea uwezo wa kiuchumi kwa kuanzisha biashara na kuwapatia kipato cha kila siku.
Mwajuma Kassima mnufaika kutoka kijiji cha Misufini kata ya Namihungo alisema, licha ya Tasaf kumwezesha kupata kipato pia imemsaidia kujenga nyumba ya vyumba vitatu anayoishi na familia yake.
Alisema, kabla ya kuanza kupokea fedha za Tasaf alikuwa na maisha duni kuishi kwenye nyumba ndogo iliyojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi jambo lililo msababishia kudharaulika mbele ya jamii,hata hivyo baada ya kuingizwa kwenye mpango wa Tasaf amekuwa mtu mwenye amani katika maisha yake na heshima kubwa ambapo ameishukuru Serikali kupitia kuleta mpango huo ambao ni mkombozi mkubwa kwa watu wanyonge.
Hata hivyo,ameiomba Serikali ifikirie upya juu ya kuongeza kiwango cha fedha kwa wanufaika kwani wapo wanaotamani kuanzisha biashara ndogo ndogo, lakini hawana mtaji kwani fedha wanazo pokea zinakidhi mahitaji ya nyumbani na kununua mahitaji ya watoto waliopo shule.
Asha Bilal,tayari amenunua bati 15 na kufyatua tofali zaidi ya elfu tatu ambazo anategemea kuanza kujenga nyumba ya kisasa ili kuondokana kuishi katika nyumba ya nyasi yeye na familia yake.
Aidha amemshukuru Rais Dkt John Magufuri kwa uamuzi wake wa kuendelea kuruhusu mpango wa kutoa fedha kwa kaya maskini kwa kuwa ni mkombozi mkubwa kwao hasa ikizinagtia kuwa baadhi ya wanufaika hawana msaada wowote.
Mkazi wa kijiji cha Namakambale ambaye ni mnufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini Tasaf Asha Mponda alisema, Tasaf imemwezesha kujenga nyumba ya kisasa,kusomesha watoto na kutokana na mradi wa ufugaji mbuzi ambapo hadi sasa ana mbuzi 8.
Ameishukuru serikali kupitia Tasaf kwa kubadilisha maisha yake,kwani imemfanya kuwa miongoni mwa watu wenye heshima kubwa katika kijiji chao.
Afisa Mtendaji wa kata ya Namakambale Hadija Lukanga alisema, kata hiyo ina kaya 391 waliopo katika mpango wa kunusuru kaya maskini kati ya hizo zipo kaya wapo ambao wameanzisha vikundi vya vya kuweka na kukopa pamoja na biashara ndogo ndogo.
Alisema, Tasaf imesaidia sana kuboresha maisha ya wananchi wa kata hiyo kwani hata kiwango cha umaskini kimepungua sambamba na mahudhurio makubwa ya watoto shuleni ambao wote wanakwenda wakiwa na sale na mahitaji yote muhimu ikilinganisha kabla ya mpango wa Tasaf.