Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, akitoa maelekezo kwa Mbunifu Majengo, Daniel Mandari (Wa pili kushoto), kutoka Wakala wa
Majengo Tanzania (TBA), ambae anasimamia ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja (OSBP), cha Kasumulu mkoani Mbeya, kuhusu ujenzi wa kituo hicho.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga (Wa Tatu kulia), akikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja (OSBP), cha
Kasumulu mkoani Mbeya. Kituo hiki kipo mpakani mwa nchi ya Tanzania na Malawi.
Mbunifu Majengo, Daniel Mandari (Wa Tatu kushoto), kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambae anasimamia ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja (OSBP), cha Kasumulu mkoani Mbeya, akimuonesha Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, ramani ya ujenzi huo.
Mbunifu Majengo, Daniel Mandari, kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambae anasimamia ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja (OSBP), cha Kasumulu mkoani Mbeya, akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu
wa Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga (Wa Pili Kushoto), alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.
Muonekano wa mradi wa ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja (OSBP), cha Kasumulu mkoani Mbeya pindi utakapokamilika. Ujenzi huo utajumuisha jengo la abiria, malori, ghala, mifugo, jengo la kupima uzito na
maegesho.
PICHA NA WUUM
********************************
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, amesema kuwa ataongea na uongozi wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) hivi karibuni ili kukubaliana
kwa pamoja kuhamisha miundombinu ya mkongo wa Taifa na umeme katika eneo la ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja (OSBP), eneo la Kasumulu mkoani Mbeya.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kipo mpakani mwa Tanzania na Malawi, Katibu Mkuu huyo amesema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kupata ridhaa kutoka kwa viongozi hao ili kuruhusu ujenzi huo kuendelea katika maeneo ambayo
mradi huo utapita mara baada ya kuhamisha miundombinu yao.
Mwakalinga, amesema kuwa mradi huo ni wa Taifa, hivyo ni muhimu kwa pande zote kukaa na kukubaliana masuala hayo bila kuathiri ufanisi wa miundombinu wa kila mmoja wao.
“Nitazungumza na viongozi wa Mashirika haya ili kuona namna ya kusaidiana kuhamisha miundombinu yao na kuruhusu ujenzi uendelee kwenye maeneo haya yenye changamoto za muingiliano wa kimiundombinu mara baada ya kukubaliana”, amesema Mwakalinga.
Amefafanua kuwa kuhusu suala la fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi huo ni kwamba Serikali inaendelea kulipa fidia hizo ambapo mpaka sasa wamebaki watu 10 ambao bado hawajalipwa na hii ni kutokana na kusubiri
mchakato wa mwisho ili nao kuweza kulipwa.
Kwa upande wake, Mbunifu Majengo, kutoka Wakala wa Majengo (TBA), Daniel Mandari, amesema kuwa mradi huo unakabiliwa na chngamoto ya uwepo wa baadhi ya miundombinu kama ya Mkongo wa Taifa na umeme katika eneo la mradi ambayo bado haijaondolewa, na
hivyo kupelekea mradi huo kusimama kwa baadhi ya maeneo.
Mandari, amefafanua kuwa mradi huo ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia na kujengwa na Mkandarasi wa Kampuni ya CGC kutoka nchini China, unagharimu Bilioni 26.4 na kwa sasa umefika asilimia 16.
Katika hatua nyingine Mwakalinga amekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kikusya – Matema Beach (Km 39.1) mkoani humo ambapo amekipongeza Kitengo cha usimamizi wa miradi cha TECU kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kuisimamia vizuri kipande cha
kilometa 4 cha barabara hiyo ambacho Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza kikamilike haraka.
Ukaguzi wa miradi hiyo ni mwendelezo wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo katika mikoa mbalimbali nchini ili kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasailiano (Sekta ya
Ujenzi).