Na John Mapepele
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Philipo Japhet Mangula amewataka watanzania kutochezea amani na kuyumbishwa na wanasiasia na badala yake waione amani walio nayo kama mtaji mkubwa wa kuwaletea maendeleo ya kweli kwa kizazi cha sasa na baadaye.
Mangula ameyasema haya leo katika ukumbi wa maktaba Manyoni wakati alipohitimisha ziara yake ya kikazi ya siku saba kwenye Mkoa wa Singida ambapo amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani ambayo imebahatika kuwa amani katika kipindi chote kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Alisema hivyo ni wajibu wa kila mwananchi mzalendo kuilinda kwa kuwa watu wengi hawapendi kuona Tanzania ina amani na kupiga maendeleo ya haraka kama inavyofanya sasa.
“Ndugu zangu hata tukichukulia mfano mdogo tu, katika kipindi cha miaka 75 ambayo tulitawaliwa na Wajerumani na Waingereza kwenye Wilaya yote ya Manyoni hatukuwa hata na Shule mmoja ya Sekondari lakini leo tuna zaidi ya shule 30 katika kipindi kifupi, je hayo siyo maendeleo makubwa ?” alihoji Mangula
Alisisitiza kuwa mapinduzi makubwa ya kiuchumi yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli yanatokana na msingi imara uliojengwa ambao ni amani na kwamba wachafuzi wa kubwa wa amani dunani kote ni wanasiasa ambao wamekuwa wakisukumwa na tamaa ya madaraka ambapo yakitokea wanaoumia ni watoto, wazee na akina mama.
Akitolea mfano wa machafuko ya kisiasa ya Rwanda ya mwaka 1994 alisema akiwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera wakati huo, alishuhudia wimbi kubwa la watoto na akina mama wakiteseka na kufa njiani wakati wakijaribu kukimbia nchi yao kunuisuru maisha yao.
“Nilishuhudia mama akina mama wakitanda kanga na kumsaidia mama mwenzao kujifungua mtoto pembeni mwa barabara na baada ya kujifungua tu wakaendelea na safari, kwa kweli huwa sipendi kukumbuka hali ile maana ni hatari na ukatili usioelezeka” aliongeza Mangula
Akiwa katika mkutano huo amesisitiza suala la uadilifu na kuzingatia sheria,kanuni na taratibu za chama cha Mapinduzi ambapo amesema vitendo vyoyote vya rushwa na wagombea kuanza kujipitisha kabla ya kipindi rasmi cha kuchukua fomu za kugombea na kuanza mchakato wa uchaguzi hakikubaliki na kusisitiza kuwa chama kitachukua hatua kwa wote watakao bainika kufanya hivyo.
Aidha Kamati za Siasa katika maeneo husika zitakazoshindwa kuwachukulia hatua wanachama watakaofanya makosa zitaadhibiwa.
Akiwa katika ziara hiyo ametembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ya Mkoa wa Singida ambapo mradi wa mwisho alioutembelea ni mradi mkubwa wa shamba la pamoja la Korosho lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 12000 eneo la Masagati kwenye Wilaya ya Manyoni na kusifu juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo kwa wananchi bila kujali itikadi ya vyama vyao.
Amesema alama ya Chama Cha Mapinduzi ni jembe na nyundo ambapo amesema jembe ni alama ya mkulima na nyundo ni mfanyakazi hivyo CCM inaamini kuwa wakulima na wafanyakazi wanamchango mkubwa katika kuchangia uchumi wa nchi yao na kuwa mapinduzi ya uchumi hapa Tanzania yameletwa na kilimo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki Mhe. Danieli Mtuka akimwelezea Mangula kwenye shamba la Korosho la Masagati ameshukuru Serikali ya Mkoa wa Singida chini ya Mkuu wa Mkoa, Dkt. Rehema Nchimbi kwa kushirikisha wananchi katika kuwabadili mawazo na mtazamo wa kutafuta maendeleo ya kweli kwa kulima shamba la pamoja la korosho ambapo amesema wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Mhe. Mtuka amesema kutokana na utafiti uliofanyika na watafiti wa kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Kilimo Naliendele kwa kushirikiana na watafiti wa mazao ya Kilimo Kanda ya Kati uliofanyika kuanzia mwaka 2002, matokeo ya utafiti huo yalionyesha kuwa hali ya hewa na udongo vinafaa kwa kilimo cha korosho hivyo wakaanza kuwahamashisha wananchi kulima zao hilo
“ Kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa na Halmashauri tuliamua kuanzisha zao la korosho kimkakati ili kuchochea kwa kasi kubwa ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja wilaya,mkoa na taifa kwa ujumla’” aliongeza Mhe. Mtuka
Aidha,alipongeza Serikali ya Mkoa kwa kubuni wazo la kuanzishwa kituo kwa kikubwa cha hija duniani cha Bikira Maria katika eneo la Sukamahela, sehemu ambayo ni katikati ya nchi ya Tanzania kwa ajili ya watu kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja kuhiji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Charles Fussi amesema kuwa kazi zinazoendelea katika eneo hilo kwa sasa ni kuhamasisha wakulima wajiunge na kilimo cha korosho, kuendelea kutoa huduma za ugani kwa wakulima ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya viuatilifu kwa kushirikiana na TARI na Bodi ya Korosho, kuendelea kazi ya kusafisha na kugawa mashamba kwa wakulima na kuzalisha miche bora korosho.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Rahabu Jackson Mwagisa amemhakikishia Mangula kuwa serikali itaendelea kusimamia kikamilifu na kuwa hamasisha wananchi kutoka sehemu mbali mbali nchini kuja kuwekeza katika kilimo cha korosho kwenye eneo hilo kwa kuwa mradi huo na manufaa makubwa kwa wananchi wa wilaya ya Manyoni na Taifa kwa ujumla.
Ametaja baadhi ya manufaa ya mradi huo kuwa ni pamoja na udhibiti wa visumbufu kama magonjwa na wadudu,udhibiti wa ubora wa korosho kutokana na usimamizi wa karibu, upatikanaji wa uhakika wa soko katika eneo la mradi,kurahisisha upatikanaji wa pembejeo na huduma za ugani ili kuhudumia eneo kubwa kwa wakati mmoja na chanzo kikuu cha malighafi za viwanda vya kusindika korosho.
Manufaa mengine ya mradi ni kuongezeka kwa mapato ya Halmashauri kupitia ushuru na kodi za biashara mbalimbali zitokanazo na ongezeko la uchumi katika sekta mtambuka zinazoendana na zao hilo, hali ya maisha kuboreka ikiwa ni pamoja na ujenzi wa makazi bora na kuongezeka uhakika wa chakula katika kaya.