Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa (kulia) akiongea na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (kushoto) alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma leo Februari 24, 2020. Ambapo pamoja na mambo mengine alipongeza uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuwateua Makamishna hao wa tume.
Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (kushoto) akimuaga Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa (kulia) mara baada ya kumaliza kikao chao kifupi kilichofanyika katika ofisi za THBUB leo,
Februari 24, 2020.
**************************
Na Mbaraka Kambona,
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) nchini umepongeza hatua ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ya kuwateua Makamishna wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora (THBUB).
Pongezi hizo zimetolewa na Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao huo, Onesmo Olengurumwa alipokutana na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu ofisini kwake jijini
Dodoma leo Februari 24, 2020.
Akiongea na Mwenyekiti huyo wa THBUB alisema kuwa uteuzi huo umefurahiwa na wadau wengi wa haki za binadamu kwani utaiwezesha tume kufanya kazi zake kama inavyopaswa.
Alisema kuwa THBUB ni chombo cha kitaifa ambacho kimeundwa kikatiba na kupewa mamlaka ya kuhamasisha na kulinda haki za binadamu nchini na wananchi wengi
wanakitegemea chombo hicho kwa ajili ya kuwasidia kutetea haki zao.
Aliongeza kwa kusema kuwa THBUB kukaa muda mrefu bila Makamishna kulikwamisha mambo mengi kwa kuwa wao ndio wenye kufanya maamuzi mbalimbali katika taasisi hiyo.
Olengurumwa alisema pia kukosekana kwa Makamishna hao kulipelekea kudorora kwa ushirikiano baina ya wadau wa haki za binadamu na taasisi hiyo, lakini sasa anaamini kwa kuwepo wao katika uongozi huduma za tume kwa wananchi zitatolewa kama inavyotegemewa.
Aidha, Olengurumwa alimuhakikishia Mwenyekiti wa THBUB ushirikiano wa karibu na kumueleza kuwa watakaa kuona maeneo gani wanaweza kushirikiana, lakini kwa kuanzia alimuahidi Jaji Mwaimu kuwa THRDC itatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa wa
tume kuhusu namna bora ya kufanya utetezi wa haki za binadamu kwa wananchi.
Akiongea mapema wakati akimkaribisha Mratibu huyo, Jaji Mwaimu alimueleza kwa ufupi kuhusu majukumu ya THBUB na mipango ya taasisi hiyo kwa mwaka huu.
Aidha mwenyekiti huyo aliahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote wakiwemo THRDC akisema kuwa tume peke yake bila kushirikiana na wadau wengine haitaweza kutimiza majukumu yake ipasavyo.
Rais John Magufuli alifanya uteuzi wa Makamishna hao mwishoni mwa mwaka jana baada ya THBUB kukaa bila Makamishna kwa takriban miaka mitatu.